Wizara ya Madini leo tarehe 10 Novemba, 2022 imeitisha kikao cha wadau muhimu kujadili mgogoro wa baina ya Mgodi wa Cata Mining Limited uliopo katika Wilaya ya Butiama na jamii inayouzunguka mgodi huo baada ya kupokea malalamiko mbalimbali kuhusu mgodi huo na mahusiano yake na jamii.
Akizungumza wakati wa kufungua kikao hicho, Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa ameutaka mgodi wa Cata Mining Limited kuwalipa wananchi waliotoa maeneo yao kupisha uwekezaji wa mgodi katika eneo hilo.
Aidha, Mheshimiwa Dkt. Kiruswa ameutaka mgodi huo kuchangia huduma za jamii kwa mujibu wa sheria za madini kwa maedeleo ya wananchi wanaouzunguka mgodi huo.
“Suala la kuchangia huduma za jamii inayozunguka mgodi ni suala la kisheria sio hisani wala msaada na linapaswa kuzingatiwa kila wakati” alisema Mheshimiwa Kiruswa.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Mara Meja Jenerali Suleiman Mungiya Mzee ameishukuru Wizara kwa kupokea malalamiko ya wananchi hao na kuitisha kikao hicho ambacho kimehudhuriwa na wadau wote muhimu katika utatuzi wa mgogoro huo.
Mheshimiwa Mzee ameahidi kuwa Ofisi yake itafuatilia kwa karibu utekelezaji wa maagizo yote ya Serikali na kuhakikisha wananchi wanaouzunguka mgodi huo wanapata stahiki yao kutoka kwa mwekezaji anayemiliki lesseni ya uchimbaji katika eneo hilo.
Kwa upande wake, Kaimu Kamishna wa Madini Bwana Msechu Mwaluvoko ameeleza kuwa katika mabadiliko ya Sheria ya Madini ya mwaka 2017, kifungu namba 105 kinachomtaka mmiliki wa lesseni za madini kuchangia huduma kwa jamii inayozunguka mgodi wa madini.
Bwana Mwaluvoko ameeleza kuwa upo mwongozo wa kuchangia huduma kwa jamii inayouzunguka mgodi ambao unamtaka mwekezaji kuandaa mpango wa kuchangia huduma kwa jamii na kuuwasilisha Ofisi ya Rais, Tawala za Miko ana Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kwa ajili ya mapitio kabla ya kuanza utekelezaji.
Kikao hicho kimehudhuriwa pia na Katibu Mkuu Wizara ya Madini Dkt. Adolf Ndunguru, Naibu Katibu Mkuu Msafiri Mbibo, Mkuu wa Wilaya ya Butiama Mheshimiwa Moses Kaegele, Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Butiama, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Butiama Bi. Patricia Kabaka.
Chanzo: Wizara ya Madini
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa