Mkoa wa Mara una eneo la Kilomita za mraba 30,150. Kati ya eneo hilo Kilomita za mraba 10,942 ni eneo la maji sawa na asilimia 36 na Kilomita za mraba 19,208 sawa na asilimia 64 ni eneo la nchi kavu. Katika eneo la nchi kavu, Kilomita za mraba 9,452.34 sawa na asilimia 49.2 ziko katika Hifadhi za wanyamapori, ikiwemo Hifadhi ya Taifa Serengeti, Mapori ya Akiba ya Ikorongo na Grumeti na Hifadhi za Jamii Grumeti na Ikorongo. Ukiondoa eneo hilo Mkoa unabakiwa na Kilomita za mraba 9,755.66 sawa na 50.7% ya eneo la nchi kavu kwa ajili ya kilimo, mifugo na makazi. Mkoa unapakana na Nchi ya Kenya na Uganda kwa upande wa Kaskazini, Mikoa ya Kagera na Mwanza upande wa Magharibi, Mkoa wa Simiyu kwa upande wa Kusini na Mkoa wa Arusha kwa upande wa Mashariki.
Kiutawala Mkoa umegawanyika katika Wilaya 6 ambazo ni; Musoma, Butiama, Bunda, Serengeti, Tarime na Rorya zenye Halmashauri 9 ambazo ni; Manispaa ya Musoma, Butiama, Bunda, Bunda Mji, Serengeti, Tarime, Rorya na Tarime Mji. Aidha, Mkoa una jumla ya Majimbo 10 ya uchaguzi ambayo ni; Rorya, Tarime Mjini, Tarime, Bunda Mjini, Bunda, Serengeti, Mwibara, Musoma Mjini, Butiama na Musoma. Makao makuu ya Mkoa ni Musoma. Kwa sasa Mkoa una jumla ya Tarafa 20, Kata 179, Vijiji 458, Vitongoji 2,504 na Mitaa 330.
Historia ya Mkoa huu inaanzia mwaka 1961 ukiwa pamoja na Mikoa ya Mwanza na Shinyanga ya sasa wakati huo ikijumuishwa kwenye EAST LAKE PROVINCE, Makao Makuu yakiwa Mwanza. Miongoni mwa Wilaya zilizounda East Lake Province ni pamoja na wilaya za North Mara na South Mara ambazo ndiyo chimbuko la Mkoa wa Mara ulioanzishwa mwaka 1963 ukiwa ni miongoni mwa Mikoa 31 ya sasa. Tangu wakati huo Makao Makuu yakawa Musoma mpaka sasa. Mkuu wa Mkoa wa kwanza akiwa Mhe.John S. Malecela kati ya mwaka 1963 hadi 1965. Tangu mwaka 1963, Mkoa umeongozwa na Wakuu wa Mikoa 17 akiwemo Mkuu wa Mkoa wa sasa Mhe. Adam Kighoma Ali Malima aliyeanza Octoba 2017.
Mkoa wa Mara ni chimbuko la Viongozi mashuhuri akiwemo Rais wa kwanza na Muasisi wa Taifa hili Hayati Mwl Julius K.Nyerere ambaye alizaliwa tarehe 13 Aprili 1922 katika kijiji cha Butiama. na kufariki na kuzikwa katika kijiji cha Butiama tarehe 14/10/1999. Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ndiye Muasisi wa Chama cha TANU kilichoongoza harakati za Uhuru. Aidha, Mwalimu alikuwa Muasisi wa Chama Cha Mapinduzi tarehe 5.2.1977 baada ya Vyama vya siasaTANU na AFRO SHIRAZI kuungana. Viongozi wengine wa Kitaifa ambao ni wazaliwa wa Mkoa huu ni Waziri Mkuu Mstaafu Mheshimiwa Jaji Joseph Sinde Warioba ambaye alikuwa Waziri Mkuu tangu mwaka 1985 hadi mwaka 1990, Wakuu wa Majeshi Wastaafu Jeneral David Msuguri na Joseph Waitara. Vile vile Mkoa huu umejaliwa kutoa viongozi wa ngazi za juu Serikalini wakiwemo Mawaziri, Mabalozi na Wakuu wa Taasisi mbalimbali za Serikali
Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2012, Mkoa ulikuwa na watu wapatao 1,743,830 ikiwa na ongezeko la asilimia 2.5 kwa mwaka na msongamano wa watu Population Density wa asilimia 80. Kwa ongezeko hilo Mkoa unakadiriwa kuwa na watu wapatao 1,989,134 (Wanaume 958,186 na Wanawake 1,030,948) hadi Desemba 31,2017.
Uchumi wa Mkoa unategemea zaidi kilimo ambacho huchangia kiasi cha 60% ya pato la Mkoa. Sekta nyingine ambazo huchangia kwenye uchumi wa Mkoa ni za Mifugo, Madini Uvuvi na Utalii. Wastani wa Pato la Mkazi kwa mwaka limekuwa likiongezeka mwaka hadi mwaka. Kukua kwa pato ghafi (GDP) la Mkoa kutoka TShs. 2,925,666,000.00 mwaka 2014 hadi TShs. 3,804,358,000.00 mwaka 2016 na pato la Mkazi kutoka TShs. 1,591,617.00 mwaka 2014 hadi TShs. 1,977,081.00 mwaka 2016 ikilinganishwa na wastani wa pato la mtu Kitaifa la TShs. 2,129,209.00 mwaka 2016 kumetokana na jitihada zinazofanyika katika kuboresha uzalishaji wa mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi. Aidha, pamekuwepo na mazingira mazuri yaliyowezesha sekta binafsi kuwekeza katika maeneo mbalimbali kama viwanda na uchimbaji wa madini.
Jedwali Na. 2 Wastani wa Pato Ghafi la Mkoa na la Mkazi kwa Mwaka (Per capita GDP)
|
Pato la Taifa
Shs. (000)
|
Pato la Mkoa
Shs. (000)
|
Pato la Mkazi Kitaifa Shs.
|
Pato la Mkazi Mkoa Shs.
|
2014 |
79,718,416 |
2,925,666 |
1,724,416 |
1,591,617 |
2015 |
90,863,681 |
3,335,364 |
1,918,928 |
1,776,538 |
2016 |
103,640,239 |
3,804,358 |
2,129,209 |
1,977,081 |
Chanzo: Ofisi ya Taifa ya Takwimu.
Makabila makuu ya Mkoa wa Mara ni Wakurya, Wajaluo, na Wajita. Wakurya ni kabila kuu la Wilaya za Tarime na Serengeti ambapo Wajita ni kabila kuu la Wilaya ya Musoma na Bunda. Wajaluo ni kabila kuu la Wilaya ya Rorya. Makabila mengine yaliyopo mkoani ni Wazanaki, Wangoreme, Wasuba, Waikizu, Waisenye, Waikoma, Wakwaya, Waluli, Washashi, Wanata na Wasweta.
Mkoa umegawanyika katika kanda tatu kijiografia kama ifuatavyo:-
Nyanda za juu; hupata mvua mara mbili kwa mwaka, wastani wa mm. 1500, zina ardhi nzuri yenye rutuba na zina wakazi wengi. Eneo kubwa la nyanda za juu liko mpakani Kaskazini Mashariki ya Wilaya ya Tarime. Shughuli Kuu ya kiuchumi katika eneo hilo ni kilimo cha nafaka hasa Mahindi, Ndizi, Viazi na Mihogo. Pia kuna mazao ya biashara ya Kahawa, Chai na Tumbaku.
Ukanda wa kati; una miinuko michache na mbuga pana zenye nyasi zinazofaa kwa malisho ya mifugo. Ukanda huu unaanzia wilaya ya Tarime na kuenea Wilaya yote ya Serengeti na kuishia Mashariki ya Wilaya ya Musoma. Hupata mvua za wastani wa mm. 1000 kwa mwaka na shughuli kuu za kiuchumi kwa wakazi wa eneo hili ni ufugaji wa Ng’ombe, Mbuzi, Kondoo na kilimo cha mazao kama vile Mahindi, Mtama, Ulezi na Mihogo.
Ukanda wa chini; katika mwambao wa ziwa unachukua sehemu kubwa ya eneo la Mkoa katika Wilaya za Bunda, Musoma na Rorya. Ukanda huu hupata mvua za wastani mm. 700 kwa mwaka na kwa kipindi kirefu cha mwaka hubakia kame. Wakazi wa eneo hili hujishughulisha zaidi na kilimo cha pamba, mihogo na nafaka. Ufugaji nao ni shughuli muhimu kama ilivyo uvuvi.
Jedwali 1.Orodha ya Viongozi wa Mikoa wa Mara
Na. |
Jina Kamili
|
Mwaka Alioanza
|
Mwaka aliondoka
|
1. |
Mhe. Adam Kighoma Ali Malima
|
2017 |
- |
2. |
Mhe. Dkt. Charles O. Mlingwa
|
2016 |
2017 |
3. |
Mhe. Magesa S. Mulongo
|
2016 |
2016 |
4. |
Mhe. Aseri Msangi
|
2014 |
2016 |
5. |
Mhe. John Tupa
|
2012 |
2014 |
6. |
Mhe. Col.(Mst.) Enos E. Mfuru
|
2009 |
2012 |
7. |
Mhe. Luteni Col. (Mst.)Issa Machibya
|
2007 |
2009 |
8. |
Mhe. Isidori L. Shirima
|
2006 |
2007 |
9. |
Mhe. Balozi. Nimrod Lugoe
|
1996 |
2006 |
10. |
Mhe. Joseph W. Butiku
|
1990 |
1996 |
11. |
Mhe. Col.Nsa Kaisi
|
1987 |
1990 |
12. |
Mhe. Augostine Mwingira
|
1982 |
1987 |
13. |
Mhe. Steven M. Wasira
|
1975 |
1982 |
14. |
Mhe. Acland Mhina
|
1967 |
1975 |
15. |
Mhe. Samwel Luangisa
|
1966 |
1967 |
16. |
Mhe. Oswald Mang’ombe
|
1965 |
1966 |
17. |
Mhe. John S. Malecela
|
1963 |
1965 |
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa