Sekta ya Maji
Utangulizi
Kwa hivi sasa inakadiriwa kuwa jumla ya watu 984,669 kati ya watu 1,893,597 sawa na asilimia 52 ya wakazi wa Mkoa wanapata huduma ya maji safi na salama. Upatikanaji wa maji vijijini umefikia asilimia 49 na mijini asilimia 54. Viwango hivyo bado viko chini ya lengo la Taifa la kufikia asilimia 65 vijijini na asilimia 90 mijini ifikapo mwaka 2015. Inategemewa kuwa viwango hivyo vitapanda baada ya kujumuisha takwimu zinazotokana na ukarabati wa miradi iliyokuwa haifanyi kazi kwa kutumia fedha za Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji (WSDP).
Halmashauri za Wilaya za Bunda, Tarime, Butiama, Musoma Vijijini, Rorya na Serengeti zinaendelea na ukamilishaji wa miradi ya maji katika vijiji kumi (10) vya awamu ya kwanza ya program ya maendeleo ya Sekta ya maji ambayo itaishia Desemba 2015.
Vyanzo vya Maji.
Vyanzo vikuu vya maji tegemezi ni vya aina kuu tatu ambavyo ni kama ifuatavyo:
i. Maji juu ya ardhi (mito,mabwawa/malambo na ziwa Victoria)
ii. Maji chini ya ardhi (visima virefu na vifupi)
iii. Maji ya mvua (uvunaji wa maji ya mvua).
Chanzo: Ofisi ya Mkuu wa Mkoa 2015
Mwenendo wa hali ya upatikanaji wa maji Mkoani Mara.
Mwenendo wa hali ya upatikanaji maji vijijini umefikia wastani wa asilimia 49 na mijini asilimia 54
Maji Mijini
Kwa upande wa Maji mijini, wakandarasi kwa ajili ya upanuzi na ujenzi wa miundo mbinu ya maji wanaendelea na kazi na wapo katika hatua mbalimbali za utekelezaji (mradi wa Musoma Manispaa 75%, Mradi wa maji Bunda Mjini 70%, Ujenzi wa chujio la bwawa la Manchira 12%, upanuzi wa mradi wa maji Tarime Mjini 75%).
Maji Vijijini
Utekelezaji wa miradi ya usambazaji wa maji vijijini (RWSSP) unaotekelezwa chini ya Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji kwa awamu ya kwanza (WSDP 1) pale ambapo vyanzo vya maji vilipatikana unaendelea na uko katika hatua mbalimbali za utekelezaji.
Uhifadhi wa Mazingira
Kutokana na juhudi zinazofanywa katika kuhifadhi mazingira, kuna mabonde muhimu sana ya uzalishaji mali endelevu kama vile; Bonde zuri la Mto Mara kwa shughuli za kilimo cha mwaka mzima, misitu ya asili inayoruhusu ufugaji nyuki wa kibiashara (wa kisasa), soko lililotayari na la uhakika kwa mazao ya bustani, mifugo na shughuli za kiutamaduni.
Changamoto
Changamoto kubwa inayoikabili Sekta ya Maji Mkoani ni shughuli za kibinadamu zinazofanyika kwenye vyanzo vya maji ikiwemo kilimo, ufugaji, uchomaji wa mkaa, ukataji miti, uchimbaji wa madini na uelewa mdogo wa wananchi juu ya uhifadhi wa vyanzo vya maji.
Mikakati iliyopo
Pamoja na kuwa na baadhi ya changamoto hizo, Mkoa ukishirikiana na Halmashauri zetu, Mamlaka na Wadau mbalimbali wanajizatiti kukabiliana na changamoto kama ifuatavyo;
i. Kutoa elimu ya afya ili kuepuka maradhi yaletwayo na ukosefu wa maji safi na matumizi ya maji yasiyo salama.
ii. Kuhimiza wananchi kuunda kamati za Maji na Usafi wa Mazingira
iii. Kuhimiza wananchi kutunza na kulinda miradi iliyopo ili iwe endelevu.
iv. Kuendelea kuhimiza wananchi juu ya umuhimu wa utunzaji wa vyanzo vya maji ili kuhifadhi wingi na ubora wa maji kwenye vyanzo hivyo.
v. Kuhimiza uvunaji wa maji ya mvua kwa kutumia mabwawa, malambo na paa za nyumba ili kupunguza uhaba wa maji kadri yanavyotumika.
vi. Kuhimiza wananchi kuchangia mifuko ya maji na kulipia huduma ya maji wanayoipata kwa wakati ili kumudu gharama za uendeshaji na matengenezo.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa