Mkuu wa Mkoa wa Mara Mheshimiwa Adam Kigoma Ali Malima amewataka viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Rorya kutumia fedha za mapato ya ndani kwenye miradi ya maendeleo.
Mheshimiwa Malima ametoa kauli hiyo leo tarehe 8 Juni 2020 wakati alipohudhuria kikao maalum cha Baraza la Madiwani kwa ajili ya kujadili hoja mbalimbali zilizotolewa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
“Badala ya kupeleka asilimia 40 ya makusanyo ya ndani kwenye miradi ya maendeleo kama mnayotakiwa kisheria, mmepeleka asilimia 6.3 tu kwenye miradi ya maendeleo, hii haikubaliki” alisema Mheshimiwa Malima.
Ameeleza kuwa kutokupeleka fedha kwenye miradi ya maendeleo kama inavyotakiwa ni kuwaonea wananchi wa halmashauri hiyo na waathirika wakuu ni madiwani ambao watarudi kwa wananchi kwenda kuomba kura.
Mheshimiwa Malima amewataka madiwani kuwasimamia watendaji ili wapeleke miradi ya maendeleo inayohitajika kwa wananchi waliowachagua.
Aidha Mheshimiwa Malima ameipongeza halmashauri hiyo kwa kufanya vizuri katika ukaguzi wa CAG kwa mwaka 2018/2019 ambapo pamoja na kupata hati safi pia walikuwa na hoja 13 mpya wakati hoja 31 zilikuwa za miaka ya nyuma.
Wakati huo huo Mkuu wa Mkoa amemtaka Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Rorya kutoa maelezo ya makubaliano kati ya halmashauri hiyo na SUMA JKT kuhusu fedha ambazo halmashauri hiyo inadai kwa SUMA JKT ifikapo tarehe 30 Juni 2020.
Mkuu wa Mkoa pia ameitaka halmashauri hiyo kuwasilisha mpango wa kulipa madeni mbalimbali ya halmashauri hiyo na ukomo wa kulipa madeni hayo kwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara.
“Mnatakiwa kumpa maelezo ya kina Katibu Tawala hili deni la bilioni 1.2 litalipwaje na kwa muda gani litalipwa” alisema Mheshimiwa Malima.
Aidha Mheshimiwa Malima aliitaka halmashauri hiyo kuimarisha mapato yatokanayo na uvuvi na kilimo cha mazao ya chakula na biashara ili kuweza kuongeza mapato ya ndani ya halmashauri hiyo.
Wakati huo huo madiwani walitumia fursa hiyo kuomba Mkuu wa Mkoa aweze kuwasaidia katika changamoto mbalimbali zinazowakabili katika kata zao.
Changamoto zilizotajwa ni pamoja na ubovu wa barabara kwa sababu barabara nyingi za halmashauri hiyo hazipitiki wakati wa mvua; kutokupatikana mawasiliano ya simu katika kata na vijiji vilivyopo katika mpaka wa Tanzania na Kenya; maombi ya fedha kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya cha Nyamagaro ambacho kimeanza kujengwa kwa nguvu za wananchi.
Changamoto nyingine ni matatizo ya umeme wa Wakala wa Umeme Vijijini (REA) ambapo madiwani walilalamikia baadhi ya taasisi na vitongoji kutokuunganishiwa umeme; maombi ya ujenzi wa madaraja; na maombi ya sekondari ya kidato cha tano na sita katika tarafa ya Nyacha.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa