Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe.Kanali Evance Alfred Mtambi leo amezungumza na wafanyakazi wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti na kuitaka Halmashauri hiyo kuanzisha mpango wa matumizi bora ya ardhi.
“Mkoa wa Mara tunalo tatizo kubwa la migogoro ya ardhi linalotokana na ongezeko la idadi ya watu huku eneo likibakia kuwa ni lile lile” amesema Mhe. Mtambi.
Kanali Mtambi amesema Mkoa wa Mara una Kilomita za mraba 30,130 na asilimia 36 ya eneo lote ni Ziwa Victoria na mito, asilimia 36.6 ni Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Mapori ya Akiba na maeneo ya Wildlife Management Area (WMA) na asilimia 27.4 tu ya eneo lote ni eneo la kilimo, makazi, ufugaji, ujenzi, taasisi, viwanda, uchimbaji wa madini na kadhalika.
Kanali Mtambi amesema kwa Sensa ya Watu na MAkazi, Mkoa una watu zaidi ya milioni 2.5 wanaongezeka kwa wastani wa asilimia 3.1 kwa mwaka jambo ambalo lisipopangiliwa litaongeza zaidi migogoro ya kugombea ardhi.
Mhe. Mtambi ameeleza kuwa kwa sasa asilimia kubwa ya wananchi wanaokuja ofisini kwake wanamgogo wa ardhi na kuitaka Halmashauri ijipange kuweka matumizi bora ya ardhi ili kupata maeneo ya malisho, mashamba ya kilimo, vyanzo vya maji na kadhalika ili kupunguza migogoro.
Mhe. Mtambi ameeleza kuwa kwa sasa kutokana na kuwepo kwa wawekezaji baadhi ya vijiji vimeanza kugombea mipaka ya vijiji na baadhi ya vijiji kuendelea kuomba Hifadhi ya Taifa ya Serengeti isogezwe jambo ambalo linaharatisha uchumi wa Taifa na taswira ya nchi katika jumuiya ya kimataifa wananchi wanapozidi kuisogelea Hifadhi.
Aidha, Mhe. Mtambi amewataka Walimu na Wakuu na Wakuu wa Shule kudhibiti maadili ya wanafunzi na watumishi mashuleni na kuwafundisha wanafunzi kwa kuzingatia weledi.
Mhe. Mtambi pia amewataka watumishi kuwahamasisha wananchi kubadilisha mfumo wa maisha na kufuga kisasa, kutumia nishati safi katika kupika na kuepuka matumizi ya kuni na mkaa.
Amewataka watumishi kusimamia miradi ya maendeleo kwa kuzingatia sheria, kanuni, taratibu na maelekezo ya Serikali katika mradi husika na kumtaka Mkuu wa Wilaya kufuatilia Kituo cha Afya Machochwe na ujenzi unaoendelea katika Hospitali ya Wilaya ya Serengeti.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Serengeti Dkt. Vincent Mashinji akizungumza katika kikao hicho ameeleza kuwa kwa sasa Wilaya ya Serengeti inatekeleza mradi mkubwa wa umeme wenye thamani ya shilingi bilioni 4.6 na mradi wa maji wa shilingi bilioni 21 katika Mji wa Mugumu.
Aidha, Mhe. Mashinji ameeleza kuwa Halmashauri imeendelea kulipa deni la watumishi wa Halmashauri hiyo shilingi milioni 500 kulingana na upatikanaji wa fedha na kwa sasa Halmashauri imedhibiti uhamishaji wa kiholela kw awatumishi.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa