Waziri wa Maji Mheshimiwa Jumaa Hamidu Aweso leo tarehe 8 Oktoba, 2022 amefanya ziara ya siku moja katika Mkoa wa Mara ambapo amezindua Bodi ya Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Musoma (MUWASA), ametembelea mradi wa maji wa Kitende na kukabidhi mradi wa maji wa Rorya- Tarime kwa mkandarasi.
Akiwa katika Wilaya ya Musoma, Mheshimiwa Aweso amezindua Bodi ya tisa ya MUWASA na kuipongeza Bodi hiyo pamoja na Menejimenti kwa kazi nzuri wanaoifanya kuboresha huduma za maji katika Manispaa ya Musoma.
Mheshimiwa Aweso amezitaka Mamlaka za maji hapa nchini kuja kujifunza MUWASA na namna ya kupandisha utendaji na molali ya wafanyakazi katika utekelezaji wa majukumu yao.
Akiwa katika Wilaya ya Rorya, Mheshimiwa Aweso ametembelea ofisi ya Chama cha Mapinduzi (CCM)Wilaya ya Rorya na kupokelewa na Mwenyekiti wa Wilaya pamoja na viongozi wengine.
Baadaye ametembelea mradi wa maji wa katika Kata ya Ktembe uliochimbwa na mdau wa maendeleo Bwana Joseph Obeyo na baadaye kukabidhi kisima hicho kwa Serikali ili iweze kusambaza maji kwa wananchi.
Akiwa katika mradi huo, Mheshimiwa Aweso ameahidi kutoa shilingi 400,000,000 kwa ajili ya ujenzi wa tenki na mtandao wa usambazaji wa maji katika eneo hilo.
Mheshimiwa Aweso pia alitembelea Kijiji cha Nyang’ombe katika Kata ya Nyamigaro ambapo alikabidhi mradi wa shilingi bilioni 134 kwa mkandarasi na kumtaka mkandarasi huyo kufanya kazi kwa ubora na haraka kukamilisha mradi huo kwa mujibu wa mkataba.
“Mimi niwahakikishie wananchi kuwa Wizara ya Maji haitacheka na mkandarasi, itacheka na maji” alisema Mheshimiwa Aweso.
Aidha, Mheshimiwa Aweso amewaahidi wananchi wa kata 10 za Wilaya ya Rorya na kata 8 za Wilaya ya Tarime kuwa mradi huo unatarajiwa kukamilika ndani ya miezi 30 kuanzia sasa na baada ya hapo wategemee kupata maji safi na salama ya uhakika.
Mheshimiwa Aweso amewataka wananchi kutoa ushirikiano kwa mkandarasi na wataalamu wanaosimamia mradi huo ili ukamilike kwa haraka waweze kupata maji kwa haraka zaidi.
Akizungumza katika maeneo mbalimbali, Mbunge wa Rorya Mheshimiwa Jafari Chege amemshukuru Mheshimiwa Waziri kwa kukamilisha miradi yam aji iliyokuwa imekwama kwa muda mrefu katika Wilaya ya Rorya.
Aidha Mheshimiwa Chege amemuomba Waziri kuruhusu mradi unavyoendelea kujengwa, wananchi wanaoishi karibu na chanzo cha maji kuanza kupata maji kabla mradi mzima haujakamilika.
Katika ziara hiyo, Mheshimiwa Waziri aliambatana na Wakuu wa Wilaya za Musoma, Tarime na Rorya, Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara, viongozi na menejimenti ya MUWASA, Wakala wa Maji Vijijini (RUWASA) pamoja na baadhi ya mameneja wa mamlaka za maji za Kanda ya Ziwa.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa