Waziri wa Madini Mheshimiwa Dotto Biteko amepiga marufuku uchimbaji wa madini usiku kwa wachimbaji wadogo katika Mgodi wa Irasanilo uliopo katika eneo la Buhemba katika Wilaya ya Butiama Mkoa wa Mara.
Mheshimiwa Biteko ametoa agizo hilo leo tarehe 12 Juni 2020 wakati alipokuwa anazungumza na wachimbaji na wananchi wa eneo la Buhemba kufuatia ajali iliyotokea katika eneo hilo na kuua wachimbaji wawili na wengine nane kujeruhiwa usiku wa kuamkia leo.
“Kuanzia sasa shughuli zote za uchimbaji katika eneo hili zifanyike mchana ni marufuku kufanyika usiku” alisema Biteko. Aidha amemtaka mwajiri wa wachimbaji waliofariki na waliojeruhiwa katika ajali hiyo kulipa fidia, kugharamia matibabu, mazishi na msiba kwa mujibu wa sheria.
Mheshimiwa Biteko aliwataka wananchi na viongozi wa mgodi huo kuheshimu sheria za nchi na kuzifuata na kupunguza migogoro isiyokuwa na tija baina ya wachimbaji na viongozi wa mgodi.
Aidha ameutaka mgodi huo kuchangia katika miradi ya maendeleo katika vijiji vinavyowazunguka kwa mujibu wa sheria. “Kuanzia kesho mgodi huu uanze kulipa mrahaba kwa mujibu wa sheria ili vijiji navyo viweze kupata chochote kutokana na uwepo wa mgodi hapa”. Alisema Biteko.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mara Mheshimiwa Adam Kighoma Ali Malima ameeleza kuwa serikali ya Mkoa wa Mara imejipanga vizuri katika kushughulikia watu wote wanaofanya ubabe katika mgodi huo.
“Nimeambiwa katika mgodi huu kuna wababe hapa ambao wanajifanya kuwa wao ndio serikali sasa sisi katika Mkoa wa Mara tumejipanga vizuri, tutawanyoosha” alisema Malima.
Mheshimiwa amewataka wachimbaji hao kuchimba madini na kutafuta riziki yao vizuri kwa kufuata sheria na taratibu za nchi.
“Mimi ninatamani pawepo na uongozi unaoeleweka na kuheshimiwa na wote ili hata sisi wengine tuusikilize huo na sio kila mtu anakuwa kiongozi katika eneo hili” alisema Malima.
Mgodi wa Isaranilo unamilikiwa na wachimbaji wadogo wadogo na tayari una lesseni 15 ambazo zinatambulika kisheria lakini kwa siku za hivi karibuni umekumbwa na migogoro baina ya wachimbaji na wasimamizi wa mgodi huo.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa