Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Nape Nnauye amefanya ziara katika Mkoa wa Mara kwa ajili ya kukagua ujenzi wa miundombinu ya mawasiliano katika Mkoa huo.
Akizungumza baada ya kuwasili Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara, Mhe. Nnauye lengo la ziara hiyo ni kukagua minara ya mawasiliano ili kuwawezesha wananchi kupata huduma za mawasiliano ambapo amesema katika Mkoa wa Mara minara 64 imejengwa na inalenga kuwafikia wananchi 284,115.
Akizungumzia umuhimu wa Serikali kuwekeza katika ujenzi wa minara ya mawasiliano Mhe. Nnauye amesema “Asilimia kubwa ya wananchi wanakaa maeneo ya vijijini na Serikali haiwezi kuyaachia makampuni ya simu kuweka minara katika maeneo hayo na wananchi ni lazima wapate mawasiliano, hivyo inatubidi kuwekeza kwenye minara”.
Mhe. Nnauye amesema lengo la Serikali ni kuhakikisha kuwa mwaka 2025 watanzania wa mijini na vijijini wapate mawasiliano kwa urahisi.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Mara ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Butiama Mhe. Moses Kaegele amesema Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) linaendelea kuimarisha hali ya upatikanaji wa mawasiliano katika Mkoa wa Mara kwa kutekeleza miradi ya kimkakati ikiwa ni pamoja na kujenga mkongo wa taifa.
Ameeleza kuwa mpaka sasa TTCL imefanikiwa kuunganisha wateja 351 katika huduma za faiba mlangoni huku wateja 346 wakiendelea kusubiri kuunganishiwa huduma hiyo.
Mhe. Kaegele amesema Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) umejenga na kukamilisha minara miwili na mingine ujenzi wake ukiwa unaendelea katika wilaya za Rorya, Tarime na Serengeti.
Katika ziara hiyo, Mhe. Nnauye ametembelea maeneo ya Kilongwe, Wilaya ya Rorya kukagua mnara unaojengwa na UCSAF ili kuboresha mawasiliano ya wananchi katika eneo hilo.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa