Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb.) leo ameiagiza Taasisi ya Kudhibiti na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kuwafuatilia na kuwachukulia hatua watumishi wa Wilaya ya Butiama waliohusika na matumizi ya fedha za Serikali kinyume na utaratibu.
Akizungumza na watumishi na viongozi wa Wilaya ya Butiama katika kikao kilichofanyika katika Ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Butiama, Mhe. Majaliwa amesema katika wizi huo viongozi wa OR-TAMISEMI, Baraza la Madiwani na viongozi wengine wa Wilaya ya Butiama hawakuweza kuubaini.
“Tarehe 13 Juni, 2022 Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Butiama aliandika barua kwenda Hazina kuwajulisha kuwa kutakuwa na fedha za ziada shilingi 736,228,732 ambazo wanaomba kibali wazihamishe na kabla ya kupata kibali aliyekuwa Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo akahamisha shilingi milioni 886, shilingi milioni 150 iliongezwa na wahasibu kwa kutumia vibali walivyokuwa navyo “amesema Mhe. Majaliwa.
Mhe. Majaliwa amesema Julai, 2022 Halmashauri ilituma shilingi 306 lakini baadaye wakarudisha Hazina shilingi milioni 98 zikabakia milioni 208 bila kulijulisha Baraza la Madiwani, wakuu wa Idara na Vitengo vingine kuhusu kuwepo kwa fedha hizo na baadaye shilingi milioni 151 zilitumika katika maeneo ambayo tayari Halmashauri ilikuwa na bajeti.
“Fedha hizo zilitumika kwenye TASAF, Sensa ya Watu na Makazi, AMREF, kupanga na kupima ardhi, marejesho ya mishahara na shilingi milioni 12 ununuzi wa vifaa vya nyumba ya Mkurugenzi” amesema Mhe. Majaliwa.
Mhe. Majaliwa amesema haya matumizi yote yalikuwa ni njia ya kutolea fedha hiyo na ndio maana orodha yake haikupelekwa kwenye Baraza la Madiwani.
Aliyekuwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Butiama alipoulizwa na Timu iliyoundwa na Ofisi ya Waziri Mkuu alisema hakuwa na taarifa ya uwepo wa fedha hizo na shilingi milioni 57 ambazo bado zilikuwepo katika akaunti zilizuiwa nab ado zipo.
Kikao hicho kimehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali, Chama cha Mapinduzi na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Butiama.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa