Wavuvi wa Halmashauri ya Wilaya ya Musoma wamesalimisha zana haramu za uvuvi 1,407 zenye thamani ya shilingi 162,630,0000 baada ya kuelimishwa kuhusu madhara ya kutumia zana hizo.
Hayo yameelezwa leo tarehe 25 Juni 2021 na Kaimu Afisa Mifugo na Uvuvi wa Halmashauri ya Wilaya ya Musoma Bwana Mbuni Oyondi wakati akisoma taarifa ya zana haramu zilizokuwa zinahitaji kuteketezwa kwa Kiongozi wa Mbio za Mwenge Kitaifa.
“Nyavu hizi zimesalimishwa na wananchi kwa hiari baada ya kupatiwa elimu ya mara kwa mara kutoka kwa wataalamu wa uvuvi kwa kushirikiana na vikundi vya ulinzi shirikishi wa rasilimali za uvuvi” ameeleza Bwana Oyondi.
Kwa mujibu wa Bwana Oyondi, kati ya zana haramu zilizosalimishwa makokoro ya sangara ni 55, nyavu za plastiki (timba) ni 1,330 na nyavu ndogo chini ya nchi sita 22.
Bwana Oyundi ameeleza kuwa Halmashauri hiyo inawahamasisha wavuvi kujiunga kwenye vikundi vya ushirika ili kuwa na uvuvi endelevu.
“Tangu Januari 2021 hadi Mei 2021 vikundi 21 vya wavuvi vimepatiwa elimu ya ushirika na tayari vikundi vinne vya ushirika vya wavuvi vimesajiriwa, vikundi vitatu vipo katika hatua za awali za usajiri” ameeleza Bwana Oyundi.
Kwa mujibu wa Bwana Oyundi Halmashauri inategemea kuwa ushirika wa wavuvi utakuwa chachu ya kulinda na kuendeleza rasilimali za uvuvi.
Ameeleza kuwa katika Mwaka wa fedha 2019/2020 sekta ya uvuvi iliingiza shilingi 849,730,384 ambayo ni sawa na asilimia 60 ya mapato ya ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Musoma.
Halmashauri ya Wilaya ya Musoma ina jumla ya wavuvi 8,263 wanaovua katika vijiji 40 vinavyozunguka Ziwa Victoria.
Akizungumza wakati wa kuteketeza nyavu hizo Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Lt. Josephine Paul Mwambashi amewapongeza sana wavuvi kwa kusalimisha zana haramu kwa hiari.
“Ninaomba niwapongeze sana kwa uamuzi wenu wa kusalimisha zana haramu za uvuvi, kitendo hiki ni kikubwa na kinahitaji kuigwa na wavuvi wengine hapa nchini” amesema Bibi Mwambashi.
Mwenge wa uhuru ukiwa katika Wilaya ya Musoma umeweka jiwe la msingi katika zahanati ya Kamunyonge; umeweka jiwe la msingi katika bweni la wanafunzi wenye mahitaji maalum katika Shule ya Msingi Mwisenge; na umetembelea mfumo wa Benki Kuu wa usajiri wa vikundi vya huduma ndogo ya fedha.
Aidha Mwenge wa Uhuru umeweka jiwe la msingi katika mradi wa maji wa Etaro; umeweka jiwe la msingi jengo la utawala katika Sekondari ya Kigera Etuma; na kuteketeza zana za uvuvi haramu na kupanda miti katika Sekondari ya Kigera Ituma.
Baada ya hapo Mwenge wa Uhuru umetembelea mradi wa kitalu nyumba na kuweka jiwe la msingi katika karakana za ufundi katika Chuo cha Maendeleo ya Wananchi (FDPC) Musoma; na kutembelea kiwanda kidogo cha kutengeneza sabuni cha wanawake na kiwanda cha kutengeneza viatu cha vijana.
Aidha mkesha wa Mwenge unaendelea katika Shule ya Msingi Nyakato iliyopo katika Manispaa ya Musoma na kesho utakabidhiwa katika Wilaya ya Butiama.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa