Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara Bwana Albert Gabriel Msovela amewataka watumishi wa Ofisi ya Mkoa wa Mara kuzingatia maadili na taratibu za kiutumishi katika utendajikazi wa kila siku.
Bwana Msovela ametoa kauli hiyo leo tarehe 29 Julai 2021 wakati alipokutana na wafanyakazi katika kikao cha kawaida cha wafanyakazi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara kilichofanyika katika ukumbi wa uwekezaji.
“Kila mtu atimize majukumu yake katika nafasi yake kulingana na sheria, taratibu na kanuni za utumishi wa umma” alisema Bwana Msovela.
Amewataka watumishi kuzingatia mazuala mbalimbali ikiwa ni pamoja na nidhamu katika utumishi wa umma na utendaji kazi kiufanisi ili kuleta tija katika kazi zao.
Aidha amewataka kuimarisha ushirikiano na mawasiliano kati ya viongozi na watumishi wa ofisi hiyo katika kutekeleza majukumu yao.
Bwana Msovela amewataka watumishi kulipa umuhimu suala la kujikinga na maambukizi ya UVIKO 19 katika sehemu za kazi kwa kuvaa barakoa na kunawa maji au kutumia vitakasa mikono muda wote na kuzingatia maelekezo mengine ya wataalamu wa afya.
“Niwaombe tu mjiepushe na misongamano isiyo ya lazima kwa wakati huu na kuchukua tahadhari za mara kwa mara kuhusu UVIKO 19 ili tuendelee kubakia salama” alisema Bwana Msovela.
Ameeleza kuwa Mkoa wa Mara unapakana na nchi jirani ya Kenya na Uganda na mikoa ambayo mingine inapakana pia na nchi nyingine na mwingiliano wa watu ni mkubwa sana kwa hiyo tahadhari ni muhimu kwa wakati huu.
Kikao cha Watumishi wa Mkoa wa Mara kilihudhuriwa na Katibu Tawala wa Wilaya ya Musoma, Wakuu wa Idara na Vitengo na watumishi wote wa Sekretarieti ya Mkoa wa Mara.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa