Katibu Tawala wa Mkoa wa Rukwa Bwana Msalika Robert Makungu leo amekabidhi Ofisi ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara kwa Bwana Bwana Gerald Musabila Kusaya katika ukumbi wa uwekezaji uliopo Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara.
Akizungumza katika hafla ya makabidhiano hayo, Bwana Kusaya amewataka watendaji wa Serikali Mkoa wa Mara kutimiza wajibu wao katika kuwahudumia wananchi na kutoa ushirikiano baina yao na kwa viongozi katika utendaji kazi.
“Kila mtu kwenye nafasi yake akitimiza wajibu wake, kazi yangu itakuwa rahisi sana na kama kuna jambo limeshindikana, mimi nipo na kwa pamoja tunaweza kulitatua au kutafuta suluhisho kwa viongozi wengine wa Serikali” amesema Bwana Kusaya.
Bwana Kusaya amesema heshima ambayo watendaji wa umma wanaipata inatokana na nafasi waliyoipata na kuongeza kuwa vyeo ni dhamana na inahitaji kutimiza majukumu ili kuendelea kukitendea haki na kukiheshimisha cheo kilichopo.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara pia amewataka wasimamizi wa kazi kwa nafasi mbalimbali za utumishi wa umma kuwasimamia watumishi waliochini yao na kuhakikisha wanafuata sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa umma katika utekelezaji wa majukumu yao.
Aidha, Bwana Kusaya amemshukuru Rais kwa kuendelea kumuamini na kuwashukuru viongozi, watumishi na wananchi wa Mkoa wa Mara kwa mapokezi mazuri aliyoyapata tangu alipowasili kwa ajili ya kuanza kazi katika Mkoa wa Mara.
Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Mkoa wa Rukwa Bwana Msalika Robert Makungu amewashukuru watumishi wa Mkoa wa Mara kwa ushirikiano waliompa tangu alipoanza kutekeleza majukumu yake mwezi Agosti, 2022 hadi allipohamaishwa.
Bwana Makungu amewataka watumishi kumpa ushirikiano Katibu Tawala mpya ili umsaidie kuwahudumia vizuri wananchi wa Mkoa wa Mara.
Bwana Makungu ameongelea umuhimu wa kuimarisha menejimenti za Halmashauri (CMT) ili ziweze kushauri Mabaraza ya Madiwani kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za nchi katika masuala mbalimbali.
Bwana Makungu ametumia fursa hiyo kuwakaribisha watumishi kuwekeza katika kilimo na ufugaji katika Mkoa wa Rukwa.
Hafla ya makabidhiano imehudhuriwa na wajumbe wa Kamati ya Usalama ya Mkoa wa Mara, Makatibu Tawala Wasaidizi na Wakuu wa Vitengo, Makatibu Tawala wa Wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri na watumishi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa