Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa Lt. Josephine Paul Mwambashi amewaasa watumishi wa Umma wanaohusika katika kusimamia miradi ya umma kuhakikisha wanatunza nyaraka na vielelezo vyote vya miradi hususan inayohusu matumizi ya fedha.
Kauli hiyo imetolewa kwa nyakati tofauti leo tarehe 24 Juni 2021 wakati wa mbio za Mwenge wa Uhuru zilizofanyika katika wilaya ya Rorya.
“Wataalamu hakikisheni mnatunza vizuri nyaraka zote za miradi ili hata zinapokuja kukaguliwa kusiwe na maswali mengi kuhusiana na utekelezaji wa mradi” ameeleza Mwambashi.
Amempongeza Mkuu wa Shule Sekondari ya Nyathorogo Mwalimu George Thobias Minanago kwa utunzaji mzuri wa nyaraka na vielelezo mbalimbali vinavyohusiana na ujenzi wa mradi wa vyumba viwili vya madarasa.
“Mara nyingi tunaamini wanawake ndio wasimamizi wazuri wa miradi lakini leo mwalimu ametuonyesha kuwa hata wanaume wanaweza kusimamia miradi vizuri na kutunza nyaraka vizuri, ninakupongeza sana” alisema Mwambashi
Aidha amepongeza pia uhifadhi wa nyaraka katika Kituo cha Afya Utegi kilichopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Rorya ambacho Mwenge wa Uhuru umekizindua leo.
Mwenge wa Uhuru leo umetembelea kiwanda cha viatu vya ngozi cha Credo Leather Industry; mradi wa barabara ya Tingirime hadi Nyanchabakenye; na baadaye ukazindua kiwanda cha mafuta ya kupikia ya alizeti cha Nyihita Sunflower Cooking Oil Production kilichopo katika eneo hilo hilo la Nyanchabakenye.
Baada ya hapo mwenge uliweka jiwe la msingi katika Shule ya Sekondari ya Kuruya na kuzindua madarasa mawili yaliyojengwa na Serikali na kukagua klabu ya kupambana na kuzuia rushwa katika Shule ya Sekondari ya Nyanthorogo .
Aidha Mwenge wa Uhuru umetembelea Shule ya Msingi Utegi kuangalia utunzaji wa mazingira na wakimbiza mwenge kitaifa walipata wasaa ya kupanda miti ya kumbukumbu katika viwanja vya shule hiyo.
Wakati huo huo, Kiongozi wa Mwenge wa Uhuru amekataa kuuzindua mradi wa maji katika shule ya Sekondari ya Buturi kutokana na mapungufu mbalimbali ikiwemo utunzaji wa nyaraka za mradi huo pamoja na utata katika uandishi wa madai ya malipo ambapo watoa huduma hawakutaja aina na kiasi cha bidhaa vilivyokuwa vinanunuliwa.
Amemuagiza Kamanda wa Taasisi ya Kudhibiti na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU) kuchunguza vielelezo na nyaraka za mradi huo na kutoa taarifa za awali leo jioni.
Aidha Mkuu wa Wilaya ya Rorya amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Rorya pamoja na menejimenti yake kutoa maelezo kuhusiana na utekelezaji wa mradi huo siku ya Jumatano tarehe 29 Juni 2021 ofisini kwake.
Mbio za Mwenge wa Uhuru katika wilaya ya Rorya zimehitimishwa jioni hii kwa mkesha wa mwenge ambao unafanyika katika mji wa Utegi na kesho unatarajiwa kukabidhiwa katika Wilaya ya Musoma.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa