Jumla ya watoto 481,104 wenye umri wa miezi tisa hadi miaka mitano wanatarajiwa kupatiwa chanjo ya magonjwa ya Surua na Rubella katika Mkoa wa Mara kuanzia leo tarehe 15 Februari, 2024 hadi tarehe 18 Februari, 2024.
Akizindua zoezi la utoaji wa chanjo hiyo katika Kituo cha Afya Nyasho, Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Said Mohamed Mtanda amesema chanjo hiyo ni salama na muhimu sana kwa watoto na amewapongeza wazazi na walezo na waliojitokeza kuwaleta watoto kupata chanjo.
“Ninawapongeza zaidi akina Baba ambao wamefika hapa kwa ajili ya kuleta watoto kupata chanjo kwa kuonyesha mfano mzuri katika jamii kwa kuzingatia mambo muhimu katika malezi ya watoto, ikiwemo chanjo” amesema Mhe. Mtanda.
Mhe. Mtanda amewataka wananchi kuhakikisha watoto wote wenye umri wa kupata chanjo hiyo wanapata na kuzingatia ushauri unaotolewa na wataalamu wa afya kuhusu chanjo na masuala ya afya kwa ujumla kwani mtoto asiyepata chanjo zote ni hatari kwa afya yake na afya ya wengine wanaomzunguka.
Mhe. Mtanda ameeleza kuwa kama kauli mbiu inavyosema “onesha upendo mpeleke mtoto akachanje”amewataka wazazi, walezi na jamii kuonyesha upendo wao kwa watoto kwa kuhakikisha wanapata chanjo hii muhimu.
Mkuu wa Mkoa amewataka viongozi wa ngazi za vijiji, Kata, Tarafa na Wilaya kutoa ushirikiano kwa wataalamu wa Sekta ya Afya ili kuweza kufanikisha zoezi la chanjo katika Mkoa wa Mara.
Wakati huo huo, Mkuu wa Mkoa amewapongeza watumishi wa Kituo cha Afya Nyasho, Manispaa ya Musoma kwa kazi yanayoifanya katika kuhudumia idadi kubwa ya wagonjwa ikilinganishwa na idadi ya watumishi waliopo katika kituo hicho.
Mhe. Mtanda amewataka kuendelea kutoa huduma wakati Serikali inaendelea kukarabati na kuboresha Hospitali ya Manispaa ya Musoma ambayo inatarajiwa kupunguza idadi ya wagonjwa wanaotibiwa katika Kituo cha Afya Nyasho.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Mkuu wa Wilaya ya Musoma Mhe. Dkt. Khalfani Haule ameeleza kuwa Wilaya ya Musoma inatarajia kutoa chanjo kwa watoto 86,000 ambapo kati ya watoto hao Manispaa ya Musoma inatarajiwa kuchanja watoto 29,000 na Halmashauri ya Wilaya ya Musoma inatarajia kuchanja watoto 57, 000.
Dkt. Haule amemshukuru Mkuu wa Mkoa kwa kuchagua kuzindua chanjo hiyo Kimkoa katika Wilaya ya Musoma na kwa kutenga muda na kushiriki katika uzinduzi huo.
Uzinduzi huo umehudhuriwa na Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Mara Dkt. Zabron Masatu; Meya wa Manispaa ya Musoma Mhe. William Gumbo, mwakilishi kutoka Wizara ya Afya, watumishi kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara na watumishi wa Manispaa ya Musoma.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa