Mkuu wa Mkoa wa Mara Mheshimiwa Ally Salum Hapi amewataka watendaji wa Mkoa wa Mara kuacha alama chanya katika utendaji wao ili kuhakikisha Mkoa unatimiza majukumu yake kama unavyotegemewa.
Mheshimiwa Hapi ameeleza hayo wakati Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mheshimiwa Eng. Robert Gabriel Luhumbi alipokuwa anakabidhi ofisi kwa Mkuu wa Mkoa wa Mara leo tarehe 12 Julai 2021 katika hafla iliyofanyika katika ukumbi wa Uwekezaji uliopo katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara.
“Leo wewe upo pale kama kiongozi wa wilaya au halmashauri, kesho umeondolewa utakuwa umeacha nini? Utaacha alama gani ili watu wakiiona wakukumbe nayo? …tuwe na nia ya pamoja viongozi na watendaji wote kila mmoja ahangaike kuujenga Mkoa wa Mara” amesema Mheshimiwa Hapi.
Ameeleza kuwa vyeo walivyonavyo viongozi na watendaji wote ni dhamana na wamepewa ili kuwaletea maendeleo wananchi wa Mkoa wa Mara na sio kuwa sehemu ya kukwamisha miradi ya maendeleo ya wananchi wa Mkoa wa Mara.
“Lazima watendaji na wananchi wetu wabadilike, wakubali kuwapokea wawekezaji……. lazima tuyaangalie manufaa mapana zaidi ya uwekezaji ambayo ni pamoja na ajira, mapato kwa halmashauri, kuimarisha mzunguko wa fedha wa eneo husika nakadhalika” alisema Mheshimiwa Hapi.
Ametoa mfano wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti ambayo ilipata fedha shilingi bilioni 1.2 kutoka Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (TANAPA) kwa ajili ya kujenga Uwanja wa Ndege wa Mugumu ili kupunguza ndege zinazotua ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti lakini mradi huo umekwama kutokana na urasimu.
“Leo hii uwanja huo ungekamilika mahoteli katika Mji wa Mugumu yangeongezeka, watalii wangekuwa wanashuka pale, halmashauri na serikali zingekusanya kodi ya mapato lakini kutokana na urasimu hayo yote hayajafanyika” ameeleza Mhe. Hapi.
Ameeeleza kuwa uongozi wa Mkoa haupo tayari kukwamishwa na watendaji wachache ambao lengo lao ni kutafuta ulaji na mazingira ambayo yanalazimisha wawekezaji kutoa rushwa na kuchelewesha wawekezaji wanaotaka kuwekeza katika Mkoa wa Mara.
Amezitaka Halmashauri kutenga maeneo ya uwekezaji mbalimbali ili kurahisisha wanapopata maombi ya uwekezaji kutoa maeneo yanayohitajika.
Aidha amewataka wananchi kuacha mara moja tabia ya kutegesha katika maeneo yanayochukuliwa kwa ajili ya uwekezaji jambo ambalo linaweza kuzuia wawekezaji na badala yake amewataka wananchi kutoa ushirikiano kwa wawekezaji ili kuweza kunufaika na uwekezaji huo.
“Ni lazima wananchi wetu wawe tayari kuwapokea wawekezaji… niwaombe viongozi wa dini mtusaidie kuendelea kuwahamasisha wananchi wawe na mazingira rafiki ya kupokea wawekezaji wanaokuja kuwekeza Mara” alisema Mheshimiwa Hapi.
Ameeleza kuwa moja ya mambo yaliyousaidia Mkoa wa Arusha kuvutia wawekezaji ilikuwa ni mwitikio wa viongozi na wananchi katika kuwapokea wawekezaji mbalimbali na kuwapa ushirikiano.
Mheshimiwa Hapi ameelezea adhma yake ya kuwahamasisha wafanyabiashara wakubwa wa Mkoa wa Mara waliowekeza katika maeneo mbalimbali hapa nchini kuwekeza miradi yao katika Mkoa wa Mara ili kukuza uchumi wa Mkoa wa Mara.
Ameeleza kuwa Mkoa wa Mara unafursa za uwekezaji nyingi ambazo zinahitaji wawekezaji wakubwa, wakati na wadogo katika madini, utalii, uvuvi, ufugaji, kilimo na kadhalika.
Ametoa mfano kuwa asilimia 70 ya Ziwa Victoria lipo katika Mkoa wa Mara wakati asilimia 30 iliyobakia ndio wanagawana mikoa ya Simiyu, Mwanza, Geita na Kagera lakini Mara haina viwanda vya samaki na uwekezaji mwingine katika sekta ya uvuvi jambo ambalo ameahidi kuanza kilifanyiakazi.
Mheshimiwa Hapi ameeleza kuwa mbali na raslimali hizo Mkoa wa Mara pia unalima mazao mengi ya biashara, mfano kahawa ya Arabica ambayo ameeleza kuwa ina ubora wa hali ya juu katika bara la Afrika lakini hamna kiwanda cha kahawa.
Akizungumza kabla ya Makabidhiano hayo, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mheshimiwa Eng. Robert Gabriel Luhumbi ameeleza kuwa kwa muda mfupi aliyokaa Mara ameona fursa kubwa sana katika Mkoa wa Mara na zikitumika mkoa utakuwa na uchumi mzuri.
“Mimi na watu wangu wa Mwanza tunatarajia kuja Mara kujifunza ufugaji wa Samaki kwenye vizimba katika Ziwa Victoria, hii ni fursa kubwa sana ya kiuchumi kwa wananchi wa Kanda ya Ziwa na nimefurahi Mara mnaitekeleza vizuri sana” alisema Mheshimiwa Luhumbi.
Mheshimiwa Hapi amehamishiwa Mara kuchukua nafasi ya aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mara Mheshimiwa Mhandisi Robert Gabriel Luhumbi ambaye amehamishiwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza baada ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kufanya mabadiliko tarehe 11 Juni 2021.
Makabidhiano hayo pia yalihudhuriwa na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa, Viongozi wa Wilaya, Halmashauri, viongozi wa dini, watendaji wa Sekretariati ya Mkoa wa Mara, wakuu wa taasisi za umma na waandishi wa habari.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa