Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Bwana Sahili Nyanzabara Geraruma amewakumbusha wataalamu wa Halmashauri wajibu wao katika kusimamia miradi ya maendeleo ya wananchi na sio kuziachia kamati za utekelezaji wa miradi ambazo hazina utaalamu.
Bwana Geraruma ametoa kauli hiyo wakati akikagua miradi ya maendeleo katika maeneo mbalimbali ya Halmashauri ya Mji wa Tarime leo na kubaini usimamizi usioridhisha na kusababisha dosari ndogondogo kwenye baadhi ya miradi ya maendeleo.
“Haiwezekani wataalamu kushindwa kusimamia miradi ya maendeleo na kuziachia kamati za usimamizi wa force account ambazo wajumbe wake sio wataalamu katika kamati walizoteuliwa kuingia” alisema Bwana Geraruma.
Bwana Geraruma amewakumbusha wataalamu kuwa serikali imewaajiri ili utaalamu wao utumike kusimamia miradi ya maendeleo yenye manufaa kwa wananchi na kutoa huduma bora kwa wananchi watu wengine kwenye hizo kamati wanakuja kuwasaidia tun a kupata ushirikishwaji wa wananchi katika utekelezaji wa miradi hiyo.
Aidha Bwana Geraruma ameshauri kamati za usimamizi wa ujenzi ziwe na wataalamu wanaohusika kama wenyeviti na katibu na wananchi wa kawaida wawe wajumbe tu katika kamati za usimamizi wa miradi hiyo.
Mwenge wa Uhuru leo umekimbizwa katika Halmashauri ya Mji wa Tarime ambapo umeweka jiwe la msingi katika mradi wa maji wa Sabasaba; umezindua klabu ya wapinga rushwa katika Shule ya Sekondari ya Nkende na umeweka jiwe la msingi katika mradi wa ujenzi wa Shule mpya ya Sekondari katika eneo la Gicheri.
Aidha Mwenge wa Uhuru umeweka jiwe la msingi katika mradi wa ujenzi wa Kituo cha Afya Ketare, umetembelea kikundi cha vijana katika barabara ya Nyamwaga na kutembelea mradi wa Halmashauri wa kufyatua tofali.
Mkesha wa Mwenge umefanyika katika Chuo cha Ualimu Tarime ambapo ukiwa hapo Mwenge ulipata nafasi ya kukagua miradi ya vikundi vya wanawake, vijana, utoaji wa elimu juu ya malaria, Ukimwi, rushwa, sensa ya watu na makazi, lishe na elimu ya kupinga dawa za kulevya.
Mwenge wa Uhuru kesho tarehe 30 Juni, 2022 utaendelea na mbio zake katika Halmashauri ya Wilaya ya Rorya.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa