Mradi wa Shule Bora kwa kushirikiana na Wakala wa Mandeleo ya Elimu Tanzania (ADEM) wameendesha mafunzo ya siku moja ya wasimamizi wa Elimu katika ngazi mbalimbaliza Mkoa wa Mara na Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti ikiwa ni kuwajengea uwezo wasimamizi wa elimu kutekeleza majukumu yao.
Akizungumza katika ufunguzi wa mafunzo kwa viongozi na wasimamizi wa shule kwa viongozi wa ngazi za Mkoa na Wilaya ya Serengeti yaliyofanyika katika Shule ya Msingi Mapinduzi A, katika mji wa mugumu, Kaimu Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Elimu na Mafunzo Bwana Ayoub Mbilinyi amewataka wasimamizi hao kutimiza wajibu wao.
Bwana Mbilinyi amewapongeza mwezeshaji wa mafunzo haya kwa kazi nzuri waliyoifanya na kuwataka washiriki kuzingatia mafunzo hayo katika utekelezaji wa shughuli zao za kila siku.
Aidha, amewasistiza wasimamizi wa ngazi zote kuwasikiliza walimu na kutatua baadhi ya changamoto zao ili walimu wafundishe wakiwa na amani, na kufanya hivyo hakuhitaji fedha wala rasilimali nyingine ni kuwasikiliza tu.
Bwana Mbilinyi ametoa mfano kuwa kuna wakati Mkoa ulikuwa na makambi ya wanafunzi katika masomo mbalimbali na walimu waliokuwa wanafundisha wanafunzi walipewa chakula tu bila posho yoyote na kazi ilifanyika vizuri.
Bwana Mbilinyi amewataka wasimamizi wa elimu walioshiriki mafunzo hayo kuyasambaza kwa maafisa wengine katika makundi tofauti tofauti ambao hawakubahatika kushiriki mafunzo hayo.
Kwa upande wake Kaimu Afisa Elimu wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti Bwana James Johannes amewakaribisha washiriki na kuushukuru Mradi wa Shule Bora na wataalamu wa ADEM kuwapitisha wasimamizi wa elimu katika mafunzo ambayo walimu wakuu wa shule za msingi watafundishwa.
“Hii ni fursa kubwa kwetu kufundishwa angalau kwa juu juu kitu ambacho watu tunaowasimamia watafundishwa kwa muda wa siku tatu, haijawahi kutokea wasimamizi wafundishwe watakachoenda kufundishwa walimu wao, tunashukuru sana” amesema Mwal. Johannes.
Aidha, Mwalimu Johannes amewataka washiriki kutumia fursa ya mafunzo haya kuongeza uelewa wao katika masuala muhimu ya kwenda kuyasimamia na kuwashukuru wakufunzi kwa kuwaelewesha kuhusu Jumuiya za kujifunza ambazo zitaundwa kwa ajili ya Walimu Wakuu na Maafisa Elimu Kata.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa