Mkuu wa Mkoa wa Mara Meja Jenerali Suleiman Mzee amewahimiza wananchi wote wa Mkoa wa Mara kushiriki kikamilifu katika zoezi la Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 ili waweze kuhesabiwa.
Akizungumza kabla ya kuhesabiwa nyumbani kwake katika Ikulu ndogo ya Musoma leo, Mheshimiwa Mzee amewataka wananchi kutoa ushirikiano kwa makarani wa sensa na kutoa taarifa sahihi ili zoezi hili katika Mkoa wa Mara liweze kwenda vizuri kama inavyotarajiwa.
“Zoezi ni muhimu sana kwa maendeleo ya Taifa letu kwa hiyo ninawaomba tusiiangushe Serikali, tushiriki kikamilifu na kujibu maswali yote ya Sensa tutakayoulizwa na makarani wa sensa” alisema Mheshimiwa Mzee.
Mheshimiwa Mzee ameeleza kuwa taarifa zote zitakazotolewa na wananchi kwa karani wa Sensa zitakuwa ni siri na zitatumika kwa madhumuni ya Sensa na makarani wote wamesaini kiapo cha kutunza siri za taarifa zote atakazozikusanya katika zoezi la Sensa.
Kwa upande wake, Mratibu wa Sensa katika Mkoa wa Mara Bwana Daniel Danda ameeleza kuwa zoezi limeshaanza vizuri katika Mkoa mzima wa Mara na tayari makarani wote wapo kwenye sehemu zao wanaendelea na kazi.
“Zoezi la Sensa limeanza rasmi usiku wa kuamkia leo, na tayari watu walio katika makundi maalum taarifa zao zimeshachukuliwa na kwa sasa makarani wanaendelea na zoezi la Sensa katika Kaya mbalimbali.
Bwana Danda ameeleza kuwa mpaka muda huo kulikuwa hamna sehemu ambapo zoezi la Sensa katika Mkoa wa Mara lilikuwa limekwama na kuwaomba wananchi kutoa ushirkiano kwa makarani wa Sensa ili kufanikisha zoezi hilo.
Zoezi la Sensa limeanza rasmi leo tarehe 23 Agosti, 2022 na litaendelea kwa muda usiopungua siku 10 kuanzia leo lakini taarifa zitakazotolewa ni za watu waliolala katika kaya usiku wa kuamkia tarehe 23 Agosti, 2022.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa