Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Bwana Sahili Nyanzabara Geraruma amewataka wananchi wa Kata ya Itiriyo iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime kuacha kulima katika chanzo cha maji ili mradi wa maji uliojengwa katika eneo hilo uweze kuleta matokeo yanayotarajiwa.
Bwana Geraruma ametoa agizo hilo leo akiwa katika eneo la Itiriyo kabla ya kuweka jiwe la msingi katika mradi wa maji wa Itiriyo.
“Ninawaasa wananchi wanaolima karibu na chanzo cha maji cha mradi huu kuacha kabisa kulima eneo hilo kwa sababu chanzo kile kinatokana na chemichemi ambayo inaweza kukauka au kutoa maji kidogo kama chanzo hicho hakitatunzwa vizuri” alisema Bwana Geraruma.
Aidha Bwana Geraruma katika maeneo mbalimbali amewakumbusha wananchi kushiriki sensa ya watu na makazi na kuachana na biashara na matumizi ya dawa za kulevya.
Bwana Geraruma amewataka viongozi wa Wilaya ya Tarime kuhakikisha wananchi wanaacha kulima mara moja katika eneo hilo ili kulinda chanzo cha maji cha mradi wa maji wa Itiriyo.
Aidha Bwana Geraruma ameitaka Wakala wa Maji Vijijini (RUWASA) kuweka uzio katika eneo la chanzo na eneo lilipo tenki la maji na pampu yam aji ili kulinda miundombinu na vifaa vilivyopo katika maeneo hayo.
Wakati huo huo, mbio za Mwenge wa Uhuru zimeendelea leo katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime ambapo ukiwa katika Halmashauri hiyo umeweka mawe ya msingi, kuzindua na kukagua miradi yote iliyokuwa imepangwa.
Miradi iliyowekewa mawe ya msingi ni pamoja na mradi wa maji Itiriyo, daraja la kebweye, Kituo cha Afya cha Bumera, na Shule mpya ya Sekondari Kata ya Sirari na umezindua Klabu ya Wapinga Rushwa katika Shule ya Sekondari ya Nyamwigura.
Aidha Mwenge wa Uhuru pia ukiwa katika Halmashauri hiyo umeteketeza madawa ya kulevya katika eneo la Turugeti-Runyerere na katika eneo la mkesha, Mwenge umekagua vikundi vya wanawake, vijana, walemavu, banda la Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) na shughuli za uhamasishaji wa wananchi kushiriki sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022.
Katika kuupokea Mwenge wa Uhuru, wananchi wengi sana walijitokeza na kubeba matawi ya miti kushangilia Mwenge wa Uhuru kuanzia eneo la makabidhiano hadi eneo la mkesha.
Mwenge wa Uhuru kesho tarehe 29 Juni, 2022 utaendelea na mbio zake katika Halmashauri ya Mji wa Tarime.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa