Zaidi ya wananchi 3,500 wa Kata ya Nyatwali, Wilaya ya Bunda wanaohama kupisha eneo la ushoroba wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti (SENAPA) leo tarehe 9 Septemba, 2024 wameanza kulipwa fidia zao zoezi lililoongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Bunda Mhe. Dkt. Vincent Naano Anney.
Akizungumza wakati wa kuanza kwa utoaji wa malipo ya fidia Dkt. Anney amemshukuru Rais kwa kuamua kulipa fidia za wananchi mapema ili waweze kuendelea na shughuli zao za maendeleo katika sehemu nyingine.
“Jambo hili lilichukua muda mrefu lakini sasa limefikia mwisho wake, niwaombe wananchi mkishachukua fidia muanze kufanya shughuli za maendeleo katika maeneo mapya ili kuzitumia fedha hizi kabla ya kuzitumia katika mambo yasiyo na msingi” amesema Mhe. Anney.
Aidha, amezitaka familia zenye migogoro kuhusu umiliki wa ardhi katika eneo hilo kumaliza migogoro hiyo haraka ili waweze kulipwa fidia zao na kuendelea na maisha mengine.
Kwa upande wake, Kamishna wa Uhifadhi wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) Bwana Mussa Kuji ameishukuru Serikali kwa kutoa fedha za kuwafidia wananchi wa Kata ya Nyatwali na kuwapongeza wananchi kwa kukubali kufidiwa ili kupisha shughuli za uhifadhi katika eneo hilo.
“Tuko kwenye zoezi muhimu sana, nimefurahi kuona wananchi wako tayari kufidiwa na kuruhusu kuachia eneo hili ili kutumika katika shughuli za uhifadhi” amesema Bwana Kuji.
Bwana kuji amewapongeza wananchi kwa kuonyesha umoja na mshikamano na kuongeza kuwa wananchi wengi alioongea nao wamefurahia kulipwa fidia na kwenda sehemu nyingine yenye amani na utulivu na kuondokana na usumbufu wa wanyama wakali katika makazi yao.
Bwana Kuji amesema kwa sasa ikolojia ya Serengeti imerudi nah ii itaongeza utalii kw aupande wa magharibi na inategemea kuongeza watalii milioni 5 na kuleta mapato ya dola za kimarekani bilioni 6 ifikapo 2025.
Akizungumza baada ya kukabidhiwa hundi ya malipo, Bi. Mgesi Kisuka Mchiro, Mkazi wa Mtaa wa Tamau ameishukuru Serikali kwa kutekeleza ahadi yake ya kutoa fidia na kwamba sasa familia yake itaondokana na adha ya wanyama wakali waliyokuwa wanaipata katika eneo hilo.
Kata ya Nyatwali ipo magharibi mwa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na wananchi wake wameanza kulipwa ili kupisha uhifadhi na uendelezaji wa eneo hilo ambalo ni mapito ya wanyama na hususan wakati wa kiangazi wanapoenda kunywa maji Ziwa Victoria pembezoni mwa Barabara ya Mwanza –Musoma.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa