Mkuu wa Mkoa wa Mara Mheshimiwa Ally S. Hapi amewataka wananchi wa Mkoa wa Mara kuchangamkia fursa zinazoletwa na serikali katika mkoa huu ili waweze kujiletea maendeleo yao.
Mheshimiwa Hapi ametoa kauli hiyo leo kwa nyakati tofauti tofauti baada ya kuwasili mkoani Mara kwa mara ya kwanza baada ya kuteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mara hivi karibuni.
“Mradi wa Chuo Kikuu ni mkubwa, na fedha zinazoletwa kwa ajili ya mradi huu ni nyingi sana na wananchi tukichamngamkia fursa zinazoletwa na mradi huu Butiama mpya inawezekana” alisema Mheshimiwa Hapi.
Ameeleza kuwa wanafunzi na watumishi wanaotarajiwa kuja ni wengi na kutokana uwingi wa watu wenye kipato Wilaya ya Butiama itakua katika uchumi wa watu wake, mapato ya halmashauri na serikali kwa ujumla.
Mheshimiwa Hapi amesema anamshukuru Mungu kwa kuhamishiwa katika Mkoa huu wa kihistoria ambapo alizaliwa na kuzikwa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
“Nimeona kuwa Rais amenipa heshima kubwa sana kuja hapa, sehemu ambayo ni kitovu cha Baba wa Taifa, amezaliwa hapa, amekulia hapa na kuzikwa hapa, na historia kubwa aliyoiacha katika eneo hili” alisema Mheshimiwa Hapi.
Amewaahidi wazee wa Wilaya ya Butiama waliokuja kumpokea kuwa atahakikisha viongozi wa Mkoa wa Mara wanaishi fikra, maono na misingi ya Baba wa Taifa ambayo ni pamoja na uzalendo, utu, usawa na uwajibikaji katika utendaji wao.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Butiama Mheshimiwa Anarose Nyamubi ameeleza kuwa kwa sasa ujenzi wa Chuo cha Kilimo, Sayansi na Teknolojia cha Mwalimu Nyerere unatarajiwa kuanza wakati wowote kuanzia sasa.
“Tayari Benki ya Dunia imeridhia kutoa fedha katika ujenzi wa Chuo Kikuu cha Mwalimu Nyerere cha Kilimo, Sayansi na Teknolojia ambacho makao makuu yake yapo katika Wilaya ya Butiama” amesema Mheshimiwa Nyamubi.
Mheshimiwa Nyamubi ameeleza kuwa katika fedha zilizoidhinishwa kwa sasa hamna zilizopangwa kwa ajili ya makazi ya wanachuo na watumishi hivyo amesema kuwa wananchi wa Butiama na Mkoa wa Mara kwa ujumla wanaweza kuwekeza katika ujenzi wa nyumba, hoteli na hosteli za kuwachukua wanafunzi na watumishi wa Chuo hicho.
Mheshimiwa Nyamubi ameeleza kuwa mbali na mradi huo, miradi mingine inayojengwa Butiama ni pamoja na mradi mkubwa wa Maji, mradi wa Chuo cha VETA,mradi wa hospitali mpya ya Wilaya ya Butiama na miradi mingine.
Aidha ameeleza kuwa kwa sasa Wilaya ya Butiama ina migodi ya kati miwili inayofanyakazi na Shirika la Madini nchini (STAMICO) limeanza kuufufua uliokuwa mgodi wa Meremeta ambao ulikuwa umefungwa kwa muda mrefu na ina wachimbaji wadogo wengi wa dhahabu na madini mengine.
“Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa, kwa sasa madini yanaing’arisha Butiama, na mgodi wa Meremeta ukianza utaongeza fursa zaidi kwa wananchi wa Butiama na Mkoa wa Mara kwa ujumla” alisema Mheshimiwa Nyamubi.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa