Mkuu wa Mkoa wa Mara Mheshimiwa Adam Kighoma Ali Malima amevitaka vyombo vya ulinzi na usalama mkoani Mara kuwakamata na kuwafungulia mashtaka watu wote waliohusika kwa namna moja au nyingine katika ufisadi uliofanyika katika malipo ya fidia ya eneo la Nyamongo.
Mheshimiwa Malima ametoa kauli hiyo leo tarehe 10 Juni 2020 katika mkutano wake na waandishi wa habari wa Mkoa wa Mara uliofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime.
“Mimi naagiza watu wote waliohusika kwa namna mmoja au nyingine wakamatwe au wajisalimishe wenyewe na wafunguliwe mashtaka kwa mujibu wa sheria” aliagiza Malima.
Mheshimiwa Malima amewataja wahusika wa ufisadi huu kuwa ni baadhi ya wananchi, baadhi ya viongozi wa serikali, viongozi wa vijiji, watumishi wa umma (waliohusika na kupima ardhi na kufanya tathmini), wafanyakazi wa benki zilizohusika malipo ya fidia na baadhi ya wafanyakazi wa mgodi wa Barrick North Mara.
“Hawa watu walishirikiana kwa lengo la kuiibia serikali na kujipatia mapato ambayo sio halali yao katika tathmini ambayo kwa sehemu ilikuwa tathmini hewa” alisema Mheshimiwa Malima.
“Mpaka sasa pesa iliyothibitika kuibiwa kwa malipo ya fidia hewa ni shilingi 3.3 bilioni na lengo la uchunguzi huo lilikuwa shilingi bilioni 5.1 na bado uchunguzi unaendelea” alisema Malima.
Aidha Mheshimiwa Malima amesema serikali itahakikisha kuwa kila mwenye haki atalipwa haki yake na kuwapongeza wananchi ambao walikataa kushirikiana na watu waliokuwa wanataka watoe pesa ili kuongezewa malipo ya fidia.
Ameeleza kuwa ubadhirifu huo umebainika baada ya tarehe 18 Mei 2020, siku mbili kabla ya kuanza kulipa fidia wananchi walionyesha wasiwasi na kutaka kuandaa mgomo ndipo Mkoa ulipoiagiza TAKUKURU na vyombo vya Ulinzi na Usalama kwa Mkoa wa Mara na Kanda Maalum ya Tarime na Rorya kushughulikia suala hilo.
Mheshimiwa Malima ameeleza kuwa kuna watu walioleta maombi ya fidia kwenye nyumba na mali hewa; wengine wanamalipo ya nyumba au viwanja ambavyo sio vyao na baada ya kupata pesa wakazipeleka kwa wenye maeneo; wengine wamelipwa malipo ambayo hayalingani na mali iliyopo kiuhalisia.
“Wananchi wa kawaida wasingeweza kufanya udanganyifu huu bila kushirikiana na viongozi na watumishi wa umma waliopewa mamlaka ya kusimamia zoezi la kufanya tathmini katika eneo la Nyamongo” alisema Mheshimiwa Malima.
Aidha ameeleza kuwa katika uchunguzi huo pia wamebaini baadhi ya watu ambao maeneo yao yaligawiwa kwa watu wengine na baada ya malipo wakarudishiwa fedha na wale waliowasaidia kubakiwa na kiasi kidogo.
Mheshimiwa Malima pia ameviagiza vyombo vya ulinzi na usalama mkoani Mara kuendelea na zoezi la uchunguzi ili kuweza kubaini ufisadi halisi uliofanywa katika malipo hayo ya fidia.
Mkutano huo na waandishi wa habari ulihudhuriwa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara Bibi Kalorina Mthapula, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Mara na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Tarime.
Wananchi 1639 wa vitongoji vinne vya vijiji vya Matongo na Bichune wanalipwa fidia ya jumla ya shilingi bilioni 33 kuanzia tarehe 20 Mei 2020 na tayari wengi wao wameshalipwa ambapo ndani yake TAKUKURU imebaini udanganyifu wa kiasi cha bilioni 3.3 na uchunguzi bado unaendelea.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa