Idadi ya watu wenye matatizo ya figo wanaopata huduma ya usafishaji wa damu katika vituo 47 vinavyotoa huduma hiyo hapa nchini imeongezeka kutoka 1,017 mwaka 2019 hadi kufikia 3,231 Desemba, 2023.
Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu katika maadhimisho ya Siku ya Figo Duniani ambayo kitaifa yamefanyika katika Manispaa ya Musoma, Mkuu wa Wilaya ya Tarime Kanali Maulid Sulumbu amewataka wananchi kulinda figo zao kwa kuweka utaratibu wa kupima mara kwa mara, kuzingatia ulaji bora na mitindo bora ya maisha.
“Hili ni ongezeko la asilimia 68.5 huku tafiti mbalimbali zikionyesha kuwa asilimia 7-14 ya watanzania ambao ni sawa na watu 10 kati ya 100 nchini wana matatizo ya figo na baadhi yao wanahitaji huduma ya kusafisha damu” amesema Kanali Sulumbu.
Kwa mujibu wa hotuba hiyo, wagonjwa 2,585 ambao ni sawa na asilimia 80 ya wagonjwa wote wanaougua ugonjwa wa figo hapa nchini wanapatiwa huduma za kusafisha damu wanahudumiwa na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) na kusababisha mfuko huo kuelemewa na gharama kubwa za kuwatibia wagonjwa hao.
Hotuba hiyo imeeleza kuwa gharama za matibabu kwa mgonjwa mwenye matatizo ya figo ni kati ya shilingi milioni 31 hadi milioni 46.8 kwa mwaka mmoja bila kujumuisha gharama za vipimo na usafiri kwa mgonjwa na wasindikizaji wa mgonjwa.
Ameeleza kuwa kutokana na ukubwa wa gharama za matibabu, wagonjwa ambao hawana bima ya afya ya kuwahudumia wanajikuta wakishindwa kujihudumia au wanaishia kufilisika jambo ambalo amesema linaweza kuepukika kama mtu akizingatia maelekezo ya wataalamu wa afya.
Wakati huo huo, Serikali imezindua mwongozo wa matibabu ya kusafisha damu ili kuongeza tija, kudhibiti na kuepusha usafishaji wa damu kuepukika ama kuahirishwa kwa lengo la kuboresha matibabu ya wagonjwa wenye matatizo ya figo.
Kanali Sulumbu amewataka wananchi kuendelea kujikinga dhidi ya magonjwa yasiyoambukizwa kwa kuzingatia ushauri wa wataalamu wa afya na hususan kuzingatia mazoezi, lishe na kupunguza matumizi ya pombe.
Kwa upande wake, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Dkt. Osmund Dyegura amesema kumekuwa na ongezeko la wagonjwa wa figo wanaopatiwa matibabu katika hospitali hiyo baada ya kuanza huduma za kusafisha damu.
Amesema kwa sasa hospitali hiyo ina wagonjwa wa figo wanaohudumiwa 80 ambao wanatakiwa kupatiwa huduma za kusafisha damu mara tatu kwa wiki.
Dkt. Dyegura ameeleza kuwa mkakati wa Hospitali hiyo ni kuanzisha kliniki za magonjwa yasiyoambukiza kuanzia ngazi ya vituo vya afya, Hospitali za Halmashauri na Hospitali za Rufaa.
Kwa upande wake, Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Figo kutoka Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando Dkt. Said Kanenda ameeleza kuwa kwa sasa hospitali hiyo inahudumia wagonjwa 6,000 wenye matatizo ya figo kwa mwaka ambao ni sawa na wastani wa wagonjwa 500 kwa mwezi.
Dkt. Kanenda ameeleza kuwa wagonjwa 61 ambao wanapatiwa huduma ya kusafisha damu kila siku katika hospitali hiyo ili kupunguza kiwango cha sumu walichonacho katika miili yao.
Ameeleza kuwa kwa sasa hospitali hiyo inaendelea kufanya maandalizi ya kuanza kupandikiza figo kwa wagonjwa wenye uhitaji ili kupunguza gharama za kusafiri kutoka Kanda ya Ziwa kwenda Hospitali ya Rufaa ya Benjamin Mkapa Dodoma.
Maadhimisho haya yamehudhuriwa na viongozi na wananchi mbalimbali kutoka Wizara ya Afya, Ofisi ya Rais TAMISEMI, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara na Manispaa ya Musoma na wananchi wa Mkoa wa Mara yakiwa na kauli mbiu Afya ya figo kwa wote, boresha usawa wa kufikia huduma na matumizi sahihi ya dawa”
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa