Uongozi wa Mkoa wa Mara umewataka wadau, wataalamu na wananchi kuongeza juhudi katika kuhifadhi ikolojia ya Bonde la Mto Mara kwa maendeleo ya kiutalii ya nchi za Tanzania na Kenya.
Hayo yameelezwa na Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Mara Mheshimiwa Lt. Col. Michael Mangwela Mtenjela wakati akizindua rasmi maadhimisho ya 10 ya Mto Mara mwaka 2021 katika viwanja vya Chuo cha Ualimu Tarime leo tarehe 14 Septemba 2021.
“Tunatakiwa kuongeza nguvu katika kuhifadhi ikilojia ili tuweze kuulinda Mto Mara kwa sababu hifadhi zetu za Serengeti na Masai Mara zinategemea sana uwepo wa Mto Mara na hifadhi hizi ni tegemeo la kiuchumi kwa nchi zetu za Kenya na Tanzania” amesema Mheshimiwa Mtenjela.
Mheshimiwa Mtenjela amesema wananchi wanaopitiwa na Mto Mara ni wanafuika wakubwa wa mto huu lakini hawana elimu ya uhifadhi wa mazingira hivyo ni muhimu wadau na wataalamu wakatoa elimu ya uhifadhi ili wananchi waweze kusaidia katika kutunza mto huu.
Mheshimiwa Mtenjela ameeleza kuwa katika kuadhimisha Siku ya Mto Mara mwaka 2021, Mkoa wa Mara umepanda miti 13,000 na kuweka vigingi 70 katika vijiji vya Mrito na Kerende vilivyopo katika Wilaya ya Tarime.
Mheshimiwa Mtenjela ameeleza kuwa idadi ya miti na vigingi imeongezeka ikilinganishwa na mwaka 2020 ambapo miti 2600 ilipandwa pamoja na vigingi 20 katika Wilaya ya Butiama.
“Ongezeko la upandaji miti linatokana na juhudi za maksudi zinazochukuliwa na Mkoa wa Mara katika kuhifadhi ikolojia ya Bonde la Mto Mara na Mkoa mzima wa Mara” alisema Mheshimiwa Mtenjela.
Mheshimiwa Mtenjela ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Tarime ameeleza kuwa japokuwa katika tukio la kuhama kwa nyumbu kutoka Hifadhi ya Taifa ya Serengeti kwenda Hifadhi ya Masai Mara Wilaya ya Tarime haitajwi, lakini Wanyama wakitoka Serengeti ni lazima wapite katika Wilaya ya Tarime kabla ya kuvuka mpaka.
Mto Mara unaanzia katika milima ya Mau nchini Kenya na unamwaga maji yake katika Ziwa Victoria.
Kilele cha maadhimisho ya Siku ya Mara kinatarajiwa kuwa tarehe 15 Septemba 2021 na mgeni rasmi katika maadhimisho hayo atakuwa Waziri wa Maji Mheshimiwa Jumaa Hamidu Aweso (Mb.).
Kauli mbiu ya maadhimisho ya 10 ya Siku ya Mara mwaka 2021 ni Tuhifadhi Mto Mara kwa Utalii na Uchumi Endelevu.
Uzinduzi wa maadhimisho hayo umehudhuriwa na viongozi mbalimbali kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Wizara ya Maji, Wizara ya Maliasili na Utalii, taasisi mbalimbali za serikali, viongozi wa Mkoa na Wilaya, Asasi zisizo za kiserikali, sekta binafsi na wananchi.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa