Uongozi wa Mkoa wa Mara umeyataka taasisi na mashirika ya umma yaliyopo katika Mkoa wa Mara kutoa ushirikiano kwa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) ili waweze kutoa huduma bora na endelevu.
Akizungumza katika ufunguzi wa Mkutano wa Wadau wa TEMESA katika Mkoa wa Mara uliofanyika leo katika ukumbi wa Mwembeni Complex kwa Niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mara, Mkuu wa Wilaya ya Musoma Mhe. Dkt. Khalfan Haule amesema kuwa pamoja na Serikali kufanya maboresho makubwa katika utendaji wa TEMESA, wadau wasipotoa ushirikiano na huduma haziwezi kuimarika.
“Taasisi zote zikilipa madeni yake wanayodaiwa na TEMESA kwa wakati, TEMESA itaweza kuwalipa wazabuni wake na kuimarisha utendaji wake na hivyo taasisi nazo zitapata huduma bora zinazotegemewa” amesema Dkt. Haule.
Mhe. Haule ameipongeza TEMESA kwa kuchukua hatua ya kujifanyia tathmini kwanza kabla ya kukutana na wadau ili kuwapa nafasi na wao kutoa maoni yao kuhusu shughuli zinazofaywa na wakala huyo katika maeneo yao ili waweze kuboresha.
Aidha, Mhe. Haule ameipongeza TEMESA kwa kuamua kufanya mabadiliko chanya katika utendaji wao na hususan kwa kuwekeza katika vifaa na rasilimali watu ili kuboresha huduma wanazozitoa kwa taasisi mbalimbali za Serikali hapa nchini.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa TEMESA Bwana Lazaro Kilahala ameeleza kuwa TEMESA ilianza kufanyakazi mwaka 1925 kama Idara ndani ya Wizara inayohusika na Ujenzi na baadaye kuanzishwa Wakala unaojitegemea mwaka 2006.
“Kwa sasa tumeamua kama Wakala kubadilika, na kutokana na mabadiliko hayo tumeanza kuwekeana makubaliano ya kimkataba na taasisi mbalimbali za Serikali kutoa huduma za matengenezo ya magari ikiwa ni pamoja na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na taasisi nyingine” amesema Bwana Kilahala.
Bwana Kilahala pia ameeleza kuwa kwa sasa Wakala inanunua vilainishi na vifaa vya umeme moja kwa moja kutoka kwa wazalishaji ili kupunguza gharama na kudhibiti ubora wa vifaa wanavyotumia katika matengenezo.
Bwana Kilahala ameeleza kuwa kwa sasa Wakala hiyo inzo karakana 27 na vivuko na inafanya shughuli zake kwa kusaidiana na watoa huduma walioainishwa katika maeneo mbalimbali hapa nchini.
Ameyataja majukumu ya TEMESA kuwa ni kufanya matengenezo ya magari, pikipiki na mitambo ya Serikali; kufanya matengenezo na usimikaji wa mifumo ya umeme, mabarafu, viyoyozi, na Elekroniki inayomilikiwa na Serikali; na uendeshaji na usimamizi wa vivuko vya Serikali.
Ameyataja majukumu mengine kuwa ni kutoa ushauri wa kitaalamu kwa Serikali na Umma kwa ujumla katika nyanja za uhandisi wa mitambo, umeme, na elekroniki; na kukodisha mitambo mbalimbali kama vile mitambo ya kuzalisha kokoto na mitambo ya kazi za barabara.
Kikao hiki kimehudhuriwa na Wakuu wa Wilaya, Kamati ya Usalama ya Mkoa wa Mara, Wakuu wa Idara na Vitendo, Wakurugenzi wa Serikali za Mitaa, taasisi na mashirika ya umma, wazabuni na wadau wengine wa TEMESA, Menejimenti na watumishi wa TEMESA.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa