Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Said Mohamed Mtanda leo tarehe 19 Novemba, 2023 amepokea taarifa na kukagua ujenzi wa Kituo Cha Polisi Wilaya ya Butiama kinachoendelea kujengwa katika Wilaya ya Butiama.
Akizungumza na Waandishi wa Habari mara baada ya kukagua na kupokea maelezo ya mradi huo, Mhe. Mtanda amesema “ujenzi huo mpaka sasa umegharimu shilingi milioni 366 na umejenga jengo lenye vyumba 25 vya ofisi, mahabusu sita na vyoo 13”.
Mhe. Mtanda ameeleza kuwa ziara yake ya kukagua ujenzi huo imetokana na taarifa iliyotolewa katika mitandao ya kijamii kuwa ujenzi huo umegharimu shilingi milioni 802 taarifa ambayo amesema sio sahihi kwa hatua za ujenzi wa jengo hilo zilipofikiwa kwa sasa.
Mhe. Mtanda ameeleza kuwa mradi wa ujenzi wa jengo la Kituo cha Polisi Wilaya ya Butiama, ni wa daraja Daraja B, una jengo moja lenye mita za mraba 737.2 na mpaka utakapokamilika ndio umekadiriwa kutumia shililingi milioni 802.
Aidha, Mhe. Mtanda ameagiza Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara kutuma wataalamu wake kufanya uchunguzi wa mradi huo Jumatatu tarehe 20 Novemba, 2023 ili kuweza kubaini uhalali wa fedha zilizotumika na fedha za kukamilisha mradi huo zilizoombwa kutoka Makao Makuu ya Jeshi ya Polisi.
Akitoa taarifa kwa Mkuu wa Mkoa, Afisa Miliki wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mara Bwana Charles Mwenya ameeleza kuwa gharama za mradi huo hadi utakapokamilika itakuwa ni shilingi milioni 802 lakini mpaka sasa fedha iliyopokelewa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Mara ni shilingi milioni 500.
Bwana Mwenya ameeleza kuwa kazi zilizofanyika mpaka sasa ni kuchimba kisima cha kutunza maji, kujenga jengo na kuezeka, kuweka flemu za milango, kupiga ripu, kujenga mabenchi ya mahabusu, kufanya wiring, kuweka magriri ya madirisha na dari maalum kwenye vyumba vya mahabusu.
Bwana Mwenya ameeleza kuwa mradi huo wa ujenzi wa Kituo cha Polisi Wilaya ya Butiama umeanza rasmi tarehe 6 Mei, 2023 na unategemewa kukamilika Desemba, 2023 na unatekelezwa kwa njia ya nguvu kazi yaani force account.
Ziara hiyo ilihudhuriwa pia na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani Mhe. Jumanne Sagini ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Butiama (CCM) na Mkuu wa Wilaya ya Butiama Mwl. Moses Kaegele, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mara ASP. Salim Morcase na Kamati ya Usalama ya Wilaya ya Butiama.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa