Mkuu wa Mkoa wa Mara Meja Jenerali Suleiman Mzee leo tarehe 24 Desemba, 2022 amekabidhi zawadi kwa wahitaji wanaoishi katika vituo vitatu vya kulelea watu wanaoishi katika mazingira magumu zenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni tatu zilizotokana na michango ya viongozi na watumishi wa Mkoa wa Mara.
Akizungumza wakati wa kukabidhi msaada huo, Mheshimiwa Mzee ameeeleza wazo la kutoa zawadi hizo lilitokana na kitendo cha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kutoa zawadi kwa ajili ya wahanga wa ukatili katika Kituo cha Masanga.
“Moyo wa Mheshimiwa Rais kutoa msaada kwa vituo mbalimbali wakati huu umetuhamasisha na sisi kutoa msaada kwa wenye uhitaji wanaoishi katika vituo vingine vilivyopo katika Mkoa wa Mara” alisema Mheshimiwa Mzee.
Aidha, Mheshimiwa Mzee amewashukuru sana viongozi na watumishi wote walioitikia wito wa kuchangia fedha za kununua zawadi hizo na kuahidi wakati mwingine michango itaanza mapema zaidi na kuwashirikisha watu wengi zaidi.
Mheshimiwa Mzee amewataka wananchi kutoa msaada wa hali na mali kwa vituo vinavyohifadhi watu wanaoishi katika mazingira magumu ili viweze kuwahudumia wahitaji wengi zaidi.
Vituo vilivyopewa zawadi ya sikukuu ni pamoja na Musoma Children Home kilichopo katika Wilaya ya Musoma, Kituo cha Kulelea Wazee cha Nyabange na Kituo cha Nyumba Salama cha Matumaini ambacho kinawahifadhi watoto ambao ni wahanga wa ukatili vilivyopo katika Wilaya ya Butiama.
Zawadi za sikukuu zilizotolewa katika vituo hivyo ni pamoja na mbuzi, mchele, maharage, mahindi, pampasi, viungo, taulo za kike na sabuni.
Katika ziara hiyo, Mkuu wa Mkoa aliambatana na Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara Bwana Msalika Robert Makungu, Katibu Tawala wa Wilaya ya Butiama, Kaimu Mkurugezi wa Wilaya ya Butiama na baadhi ya watumishi kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Wilaya ya Musoma na Wilaya ya Butiama.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa