Kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru godfrey eliakimu mzava amewataka vijana kuachana na mambo yasiyo na tija wajiunge kwenye vikundi vy uzalishaji mali na kuchangamkia fursa za mikopo inayotolewa na Serikali kupitia Mamlaka za Serikali za Mitaa.
Ndugu Mzava ametoa rai hiyo wakati akizungumza na vijana baada ya kukagua mradi wa kikundi cha vijana cha Eden Group katika Kijiji cha Muriba, Kata ya Muriba Halmashauri ya Wilaya ya Tarime wakati Mwenge wa Uhuru ukiendelea na mbio zake katika Wilaya ya Tarime.
“Kikundi hiki kinaundwa na viwanja watano wenye elimu ya Chuo Kikuu na mmoja chuo cha kati ambao walijiunga na kukopeshwa shilingi milioni sita na Halmashauri ya Wilaya ya Tarime mwaka 2023 ambao mpaka sasa wamesharejesha fedha zote za Halmashauri na biashara yao inaendelea vizuri” amesema Bwana Mzava.
Kiongozi huyo wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa amewapongeza vijana hao kwa kuungana pamoja katika mambo ya kujiletea maendeleo na kuanzisha biashara ambayo inaendelea vizuri na kumtaka Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime mikopo itakapofunguliwa tena, kikundi hicho kipewe kipaumbele.
Bwana Mzava amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri kutoa kipaumbele cha mikopo kwa vikundi vinavyowahi kurejesha mikopo ya makundi ya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu ili waweze kuendelea kufanya shughuli za uzalishaji mali na kupunguza tatizo la ajira katika jamii.
Kwa upande wake, Katibu wa Kikundi cha Eden Group Bwana Amos Lameck Gisiri amesema kikundi hicho kilianzishwa mwaka 2022 na kusajiliwa na Halmashauri hiyo kikiwa na wanachama watano na kati yao wanne wakiume na mmoja wakike.
Bwana Gisiri amesema kikundi chao kinajishughulisha na biashara ya vifaa vya umeme wa majumbani na viwandani na kiliwahi kukopeshwa na Halmashauri mwaka 2023 ambapo walirejesha mkopo na kwa sasa biashara yao ina mtaji wa shilingi 7,200,000.
“Lengo la kikundi ni kuwa na kampuni kubwa ya uuzaji na usambazaji wa vifaa vya umeme Wilayani Tarime” amesema Bwana Gisiri na kuongeza kuwa kwa sasa pamoja na duka hilo wameshafungua duka jingine katika kijiji cha Gibaso na kutoa ufadhili wa elimu kwa kijana mmoja kusomea Chuo cha Lubondo Biharamulo.
Mwenge wa Uhuru unaendelea na Mbio zake katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime baada ya Katibu Tawala wa Wilaya ya Tarime Bibi Angelina Lubella Marko kukabidhi Mwenge wa Uhuru kwa Katibu Tawala wa Wilaya ya Tarime Bwana Saul Mwaisenye katika Kijiji cha Kerende, Halmashauri ya Wilaya ya Tarime.
Miradi mingine ambayo imetembelewa na kukaguliwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime ni pamoja na jengo la biashara la Nyamongo Plaza ambao umezinduliwa, mradi wa maji Nyangoto ambao umetembelewa kuangaliwa uendelevu wake baada ya kuzinduliwa na Mwenge wa Uhuru mwaka 2023, mradi wa Bweni la wanafunzi wenye mahitaji maalum katika Shule ya Msingi Nyamwaga.
Miradi mingine itakayopitiwa na Mwenge wa Uhuru leo ni nyumba ya mtumishi ya 2 in one katika Kituo cha Afya Magoto, ujenzi wa daraja la Kebweye na mradi wa uhifadhi wa mazingira katika Shule ya Sekondari ya Nyasaricho.
Mkesha wa Mwenge wa Uhuru unatarajiwa kuwa katika Uwanja wa Tarafa katika eneo la Sirari na kesho Mwenge unatarajiwa kukabidhiwa katika Halmashauri ya Mji wa Tarime.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa