Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Kazi, Ajira, Vijana na Walemavu Mheshimiwa Anthony Mavunde amewataka vijana hapa nchini kubadili mtazamo wao kuhusu ajira ili kuweza kuzifanya shughuli zao zinazowaingizia fedha kwa bidii na maarifa.
Mheshimiwa Mavunde ameeleza hayo katika Kongamano la Vijana wa Mikoa ya Simiyu, Mwanza na Mara lililoandaliwa na wizara yake kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo na wadau wengine lililofanyika katika Wilaya ya Butiama tarehe 10 Machi 2020.
Ameeleza kuwa kwa mujibu wa sera ya ajira, “ajira ni shughuli yoyote halali inayomwingizia mtu kipato”. Hata hivyo vijana wengi wanadhani kuwa ajira ni lazima aajiriwe na akae ofisini ndio waiheshimu.
Mheshimiwa Mavunde amesema serikali inampango kwa kushirikiana na wadau katika kuziibua, kuzitangaza na kuzigawa fursa kwa vijana wengi hapa nchini ili waweze kujiajiri.
Mheshimiwa Mavunde amesema vijana wengi wanakata tamaa mapema, katika shughuli zao wakipata changamoto kidogo tu wanakata tamaa. Amewataka washiriki wa kongamano hilo kulitendea haki kwa kujifunza na mwisho kuyafanyia kazi yale yote waliyojifunza.
Amewataka vijana kuchangamkia fursa za kilimo cha matunda na mbogamboga ambazo zinaonekana kuwa na soko kubwa ndani nan je ya nchi.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mara Mheshimiwa Adam Malima akizungumza kabla ya kumkaribisha Naibu Waziri kuzungumza katika kongamano hilo, amesema vijana wanayonafasi kubwa sana ya kuweza kujiajiri katika kilimo na biashara nyinginezo.
Aidha amewataka vijana kujiunga katika vikundi vya uzalishaji mali ambavyo vitawasaidia kupata mtaji, ujuzi na masoko ya bidhaa watakazozalisha.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Buatiama Mheshimiwa Anna Rose Nyamubi ameshukuru kwa waandaaji kuleta kongamano hilo katika Wilaya ya Butiama wilaya ambayo inahistoria kwa ya Taifa la Tanzania.
“Hii wilaya ndiyo wilaya ambayo Rais wa Kwanza wa Tanzania Hayati Mwalimu Nyerere alizaliwa na kuzikwa hapa” alisema Mhehsimiwa Nyamubi.
“Tunaushukuru sana uongozi wa Mkoa kwa kuamua kuleta kiwanda kikubwa cha maziwa na uwanja wa kudumu wa maonyesho ya Kilimo katika Wilaya ya Buatiama. Alisema maamuzi hayo yatatoa fursa kwa vijana wengi kupata ajira na kujifunza mambo mbalimbali kupitia fursa hizo.
Aliwataka vijana kuchangamkia fursa za kilimo, uvuvi na ufugaji ili kuweza kutengeneza kipato halali ambacho kitawawezesha kutimiza ndoto na malengo yao.
Kongamano hilo lilihudhuriwa pia na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Butiama na Chief Josephat Wanzagi, kiongozi wa Kabila la Wazanaki.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa