Mkuu wa Mkoa wa Mara Mheshimiwa Ally Salum Hapi ameelezea matumaini yake kuwa Uwanja wa Ndege wa Musoma utakapokamilika utaufungua Mkoa wa Mara kiuchumi.
Mheshimiwa Hapi ametoa matumaini hayo leo tarehe 3 Agosti 2021 wakati wa ziara yake aliyoifanya katika Manispaa ya Musoma kukagua miradi ya maendeleo.
“Huu uwanja ukikamilika ndege kubwa za abiria na mizigo zitatua hapa na hivyo kuwaleta watalii kutua Musoma halafu kuingia katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na kusafirisha samaki kutoka viwandani moja kwa moja bila kuhitajika kupitia Mwanza” alisema Mheshimiwa Hapi.
Ameeleza kuwa kutokana na utajiri mkubwa uliopo Mkoa wa Mara na miradi mikubwa inayojengwa ikiwemo Hospitali ya Rufaa ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere na Chuo Kikuu cha Mwalimu Nyerere cha Kilimo, Sayansi na Teknolojia uwanja wa ndege utafungua zaidi mirango ya kiuchumi.
Mheshimiwa Hapi ameeleza kuwa kutokana na historia ya uwanja huo kwa taifa la Tanzania, kukarabatiwa kwake ni sehemu ya kumuenzi Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ambaye alikuwa akiutumia uwanja huo mara kwa mara akiwa hai.
“Hata wakati wa vita vya Kagera, uwanja huu ulitumika katika kusafirisha wapiganaji na mizigo kwenda Uganda kwa wakati huo” alisema Mheshimiwa Hapi.
Ameahidi kufuatilia malipo ya awali ya mkandarasi katika Wizara ya Ujenzi na Usafirishaji ili kazi ya ukarabati wa uwanja huo iweze kuanza mara moja.
Hatua iliyofikia kwa sasa Mkandarasi ameleta vifaa vya ujenzi na anaendelea na ujenzi wa ofisi za muda atakazozitumia wakati wa utekelezaji wa mradi huo.
Akitoa taarifa ya Mradi huo Meneja wa TANROADS Mhandisi Mlima Ngaile ameeleza kuwa kazi zitakazofanyika ni pamoja na kukarabati njia ya kutua na kurukia ndege kuwa kiwango cha lami yenye urefu wa kilomita 1.705.
“Kazi nyingine ni ukarabati na uboreshaji wa maungio (tax way),ukarabati wa maegezo ya ndege, uzio wa usalama, ujenzi wa miundombinu ya kuondoa maji yasituame, ujenzi wa jengo la zimamoto, ununuzi wa gari la zimamoto, ujenzi wa kituo cha umeme na ununuzi wa genereta” alisema Mhandisi Ngaile.
Ameeleza kuwa kazi nyingine ni ujenzi wa jengo la muda la waongoza ndege, ununuzi na ufungaji wa mitambo ya radio call.
Mkataba ulisainiwa tarehe 28 Desemba 2020 na mkandarasi alikabidhiwa eneo la ujenzi tarehe 30 Aprili 2021 na mkandarasi alipewa miezi mitatu ya kujiandaa kwa kazi ya ujenzi ambapo ilikamilika tarehe 30 Julai 2021.
Kwa muUtekelezaji wa mradi huu kwa mujibu wa mkataba ni wa miezi 20 na utakapokamilika utaruhusu ndege kubwa za abiri na mizigo kuanza kutua katika uwanja huo.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa