Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mheshimiwa Dkt. Angelina Mabula ameeleza kuwa lengo la Serikali kulitwaa eneo la Ghuba ya Speke lenye ukubwa wa ekari 14,250 lililopo katika Kata ya Nyatwali ni kwa manufaa ya umma kwa uhifadhi endelevu wa mfumo wa ikolojia wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara na wananchi wa Kata ya Nyatwali, Mheshimiwa Mabula ameeleza kuwa hakuna mwekezaji atakayepewa eneo la Nyatwali lililopo katika Wilaya ya Bunda, pembezoni mwa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti katika barabara ya Mwanza- Musoma hadi Sirari.
“Hakuna mwekezaji anayekuja kuwekeza katika eneo la Nyatwali, hili eneo linaachwa kwa ajili ya kuunganika na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti ili kulinda ikolojia ya hifadhi na kuruhusu wanyama kupita kwenda Ziwa Victoria bila mwingiliano wowote”ameeleza Mheshimiwa Mabula.
Mheshimiwa Mabula ameeleza kuwa katika kuliendeleza eneo hilo, Serikali pia imepanga kubadilisha miundombinu ya barabara inayopita katika eneo hilo ili kupisha wanyama waweze kupita bila mwingiliano wa watu na magari.
Mheshimiwa Mabula ameeleza kuwa Serikali ya awamu ya sita haipo tayari kuona wananchi wake wanaonewa, wala kuna ukiukwaji wa haki za binadamu katika utwaaji wa eneo la Nyatwali, bali haki itatendeka na kila mwananchi atalipwa anachostahili baada ya kuridhia kuhama.
Mheshimiwa Mabula amewatahadharisha wageni kutoka nje ya eneo hilo wanaonunua maeneo katika eneo la Nyatwali ili waje kulipwa fidia na Serikali kuwa Serikali ipo makini sana katika kufanya tathmini ya waathirika wa zoezi hilo.
Kuhusu bei ya fidia, Mheshimiwa Mabula ameeleza kuwa Serikali imeangalia bei za kawaida wananchi wanazouziana maeneo katika eneo hilo na kuongeza fedha kidogo wakati serikali itakapolipa fidia, aidha bei za miti, maua na vitu vingine bei zimebandikwa ili wananchi waweze kufahamu kabla ya kuridhia kuondoka.
Mheshimiwa Mabula ameeleza kuwa serikali haipo tayari kuwadhulumu wananchi wake, watu wote watalipwa stahiki zao endapo wataridhia kuhama kwa hiari na hakuna kitakachokwenda kinyume na matarajio ya wananchi katika malipo ya fidia kwa maana ya kupata stahiki zao kama wataondoka katika eneo hilo.
Mheshimiwa Mabula ameeleza kuwa mpaka sasa kaya 630 kati ya 1,274 zimefanyiwa uthamini ambayo ni sawa na asilimia 49 na zoezi la uthamini linaendelea vizuri na ameipongeza Serikali ya Mkoa wa Mara kwa kusimamia zoezi hilo.
Mheshimiwa Mabula ameeleza kuwa Serikali inaheshimu makabuli yote yaliyopo katika eneo hilo na itahakikisha makaburi yote yanahamishwa kwa heshima na Serikali itagharimia uhamishaji wa makaburi hayo maeneo yatakayohamishiwa.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mheshimiwa Mary Francis Massanja ameeleza kuwa awali, eneo hilo lilikuwa ni Game Controlled Area lakini sasa itakuwa ni sehemu ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na kutokana na umuhimu wake inabidi binadamu wapishe.
“Kwa sasa hata idadi ya watu imeongezeka sana ukilinganisha na miaka ya 1980 ambapo eneo hilo lilikuwa na idadi ndogo ya watu na ilikuwa rahisi kwa wanyama kuishi na binadamu” alisema Mheshimiwa Masanja.
Naibu Waziri huyo amewatoa hofu wananchi wa eneo hilo kuwa yeye pia ni mmoja wa watu watakaohama kutoka eneo hilo kwa kuwa ndio nyumbani kwao na anamifugo yake katika eneo hilo lakini kwa sasa yupo tayari kuhama hiari kwa manufaa ya umma.
Mheshimiwa Masanja amewataka wananchi wa Nyatwali kukubali kwa hiari kulipwa fidia na serikali kupisha uendelezaji wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti kwa manufaa ya watanzania wote.
Akitoa taarifa kwa Mawaziri, Mkuu wa Wilaya ya Bunda Mheshimiwa Joshua Nassari ameeleza kuwa katika Wilaya ya Bunda maamuzi hayo yameelekeza utwaaji wa eneo la ekari 14,250 kwenye Ghuba ya Speke lenye mitaa minne yenye jumla ya watu 9,836 iliyomo katika Kata ya Nyatwali katika Halmashauri ya Mji wa Bunda.
Mheshimiwa Nassari ameeleza kuwa kutokana na elimu iliyotolewa wananchi wamehamasika na tayari wananchi 837 wameshachukua fomu na kujiandikisha kuondoka kwa ajili ya kuondoka katika eneo hilo.
“Tayari wananchi 502 waliojaza fomu za kuondoka katika eneo hilo wameanza kufanyiwa tathmini ambayo ni saw ana asilimia 12.4 ya lengo la kuthamini mali za wananchi 4,050 lililowekwa na Serikali” alisema Mheshimiwa Nassari.
Mheshimiwa Nassari ameitaja mitaa itakayoathirika kuwa ni Mtaa wa Tamau (3,214), Mtaa wa Serengeti (2,252), Mtaa wa Nyatwali (1,588) na Mtaa wa Kariakoo (2,782) na kuongeza kuwa eneo hilo lina shule za msingi tatu, shule za sekodari moja, zahanati moja, kituo cha afya kimoja, umeme na maji.
“Utekelezaji wa maelekezo ya Baraza la Mawaziri katika Wilaya ya Bunda umehusisha kuandaa mpangokazi wa zoezi hilo unaojumuisha shughuli za uhamasishaji, uthamini wa mali, ulipaji wa fidia, mpango wa maeneo/huduma mbadala kwa wananchi wanaohama na mpango wa uendelezaji wa eneo linalotwaliwa baada ya kulipa fidia” ameeleza Mheshimiwa Nassari.
Aidha, Mheshimiwa Nassari ameeleza kuwa uamuzi wa Baraza la Mawaziri kuhusu utatuzi wa migogoro ya matumizi ya ardhi katika vijiji 975 hapa nchini na katika Mkoa wa Mara unahusisha migogoro ya ardhi katika wilaya za Rorya, Butiama, Tarime na Bunda.
Mkutano huo pia umehudhuriwa na Mkuu wa Mkoa wa Mara Meja Jenerali Suleiman Mungiya Mzee, Naibu Waziri wa Maji MaryPrisca Mahundi, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mheshimiwa Marry Masanja, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mheshimiwa Abdallah Ulega.
Wengine waliohudhuria ni Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tawala za Miko ana Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. David Ernest Silinde, Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira Mhe. ----Naibu Waziri wa Kilimo Mheshimiwa Antony Peter Mavunde, Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara Bwana Msalika Robert Makungu na viongozi wengine wa Chama na Serikali.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa