Zoezi la uthamini katika eneo la Ghuba ya Speke, katika Kata ya Nyatwali, Wilaya ya Bunda kwa ajili ya kuimarisha uhifadhi endelevu wa mfumo wa ikolojia wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na usalama wa wananchi linaendelea vizuri na kwa sasa limefikia asilimia 53.7 ya utekelezaji wake.
Akizungumza katika Kikao cha kupokea taarifa ya utekelezaji wa zoezi la uthamini leo Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara Bwana Msalika Robert Makungu amewataka wataalamu wanaofanya uthamini huo kutoa taarifa za maendeleo ya kazi kila wiki kwenye Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara kwa ajili ya kupata uelewa wa pamoja na kutoa mrejesho wa maendeleo ya utekelezaji wa zoezi hilo Serikalini.
“Ninataka kuanzia sasa, kila wiki Mkoa upate taarifa ya maendeleo ya zoezi la uthamini ili Mkoa uweze kupeleka taarifa za utekelezaji wa uthamini na maendeleo ya zoezi hili kila wiki” amesema Bwana Makungu.
Aidha Bwana Makungu amewataka wataalamu hao kuongeza kasi ya kufanya tathmini ili zoezi hilo liweze kukamilika kwa haraka na wananchi wa eneo la Nyatwali waweze kulipwa fidia zao na kuendelea na shughuli zao za kawaida.
Taarifa ya wataalamu inaonyesha kuwa mpaka hadi kufikia tarehe 25 Januari, 2023 jumla ya wananchi 2,175 wametambuliwa na kufanyiwa uthamini kati ya watu 4,050 waliokadiriwa hapo awali ambayo ni sawa na asilimia 53.7 ya uthamini wote.
Aidha, taarifa hiyo imeeleza kuwa zoezi la uthamini lilianza Novemba, 2022 na linatarajiwa kukamilika Machi, 2023 na mpaka sasa jumla ya fomu 2,822 kati ya 4,050 zilizokadiriwa zimechukuliwa na wananchi ambayo ni sawa na asilimia 69.68 ya makadirio ya awali.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, zoezi la uthamini katika eneo hilo ni la hiari na kabla ya kuanza lilitanguliwa na mikutano na vikao vya uhamasishaji kwa viongozi na wananchi wa Kata ya Nyatwali na Wilaya ya Bunda kwa ujumla.
Utekelezaji wa uamuzi wa Baraza la Mawaziri wa kutwaa eneo la Ghuba ya Speke lenye ukubwa wa ekari 14,250 kwa manufaa ya umma unahusisha Mitaa ya Tamau, Nyatwali, Kariakoo na Serengeti iliyopo katika Kata ya Nyatwali, Wilaya ya Bunda katika Mkoa wa Mara.
Utwaaji wa eneo la Ghuba ya Speke, utaunganisha Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na Ziwa Victoria na kuongeza ukubwa, uzuri wa mandhari ya vivutio vya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.
Kikao cha kupokea maendeleo ya uthamini kimehudhriwa pia na Katibu Tawala wa Wilaya ya Bunda, Wakuu wa Idara na Vitengo vya ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara na baadhi ya wataalamu wa wanaohusika na zoezi la uthamini katika Ghuba ya Speke.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa