Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Mara Raphael J Nyanda amesema kuwa fedha zilizotolewa na Serikali kwenye ujenzi na ukarabati wa vituo vya afya lazima ifanye kazi iliyotarajiwa. Nyanda ameyasema hayo jana kwenye ziara ya ukaguzi wa Ujenzi wa Vituo vya Afya sita katika Halmashauri mbalimbali Mkoa wa Mara.
“Imekuwa ni tabia ya mazoea kuwa ujenzi wa majengo ya Serikali unafanyika hovyo hovyo pasipo kujali thamani ya fedha. Katika kipindi cha uongozi wangu sitakubali,nasema sitakubali kabisa kupokea majengo yasiokidhi viwango.Ni lazima kazi mnayoifanya iwe na ubora sambamba na fedha tuliyowapa,”alisema Nyanda akiwa anawaasa wasimamizi wa ujenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda.
Alisisitiza kuwa ujenzi huo unatakiwa kukamilika si zaidi ya tarehe 15 Mei ,2018 na uzinduzi rasmi wa kitaifa wa ujenzi wa vituo hivyo ni mwisho wa mwezi wa tano.”Hivyo basi ni lazima mhakikishe mnafanya kazi usiku na mchana pasipo kusimama ili kukamilisha kazi hiyo kwa kuwa fedha zipo na hakuna sababu ya kutokamilisha kazi kwa wakati’” alisema Nyanda.
Naye Mkaguzi Mkuu wa ndani wa Mkoa Yusuph Luhende alisema kuwa baada ya ujenzi huu kukamilika ni lazima ukaguzi wa kina ufanyike ili kujua matumizi ya fedha kama yamefanyika kwa kufuata taratibu.
“Mnatakiwa kuwa makini sana na manunuzi mnayofanya.Singatieni taratibu na kuhakikisha kila mnachokifanya ni matokeo ya kamati ya ujenzi.Mkumbuke kutunza risiti zote za manunuzi ili kutojiweka kwenye matatizo hapo badae,” alisema Luhende.
Ujenzi na ukarabati wa Vituo vya Afya ni mpango wa serikali kwa nchi nzima wa kuhakikisha kunakuwa na mazingira bora na salama ya kutolea huduma za afya.
Imetolewa na Stephano Amoni- Afisa TEHAMA
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa