Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Mara imebaini kuwepo kwa ufisadi wa bilioni 3.2 katika malipo ya fidia ya ardhi katika mgodi wa Barrick North Mara katika Wilaya ya Tarime.
Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Kamanda wa TAKUKURU Mkoa wa Mara Bwana Alex J. Kuhanda imeeleza kuwa taasisi yake imethibitisha kuwepo kwa malipo hewa yenye thamani ya shilingi 3,271,038,570.28 na uchunguzi bado unaendelea.
“Katika uchunguzi wetu kupitia tuhuma 60 tulizozifanyia kazi tumeweza kuthibitisha kuwepo kwa ufisadi mkubwa uliochochewa na uthamini uliojaa rushwa” alisema Bwana Kuhanda.
Aidha amefafanua kuwa katika tuhuma hizo 60 TAKUKURU imebaini kuwa malipo halali kwa wananchi yalikuwa shilingi 226,858,656.52 tu na sio 3,482,988,360 zilizolipwa kama fidia kwa nyumba 72 ambazo uchunguzi umethibitisha kuwa ni hewa.
Bwana Kuhanda ameeleza kuwa kati ya malipo hayo shilingi 2,127,236,784 ilikuwa ni malipo ya fidia kwa nyumba na shilingi 1,143,796,786.28 ilikuwa ni malipo ya posho ya usumbufu na kuhama kutoka katika nyumba ambazo hazipo na hazikuwahi kuwepo.
Bwana Kuhanda ameeleza kuwa msingi wa uchunguzi wa TAKUKURU ulilenga kujua kama ni kweli kulikuwa na malipo yaliyokuwa yanafanyika kwa tathmini ya mali hewa.
Kwa upande wake mwakilishi wa mgodi wa Barrick North Mara ameeleza kuwa hadi tarehe 9 Juni 2020 wananchi 1498 walikuwa wameshalipwa na wananchi 142 walikuwa bado wanaendelea kulipwa.
Ameeleza kuwa katika mchakato mzima iliundwa kamati ya usimamizi ambayo ilihusisha watendaji kutoka katika ngazi ya Mkoa, Wilaya na vijiji vilivyonufaika na fidia hiyo.
Aidha alieleza kuwa Mgodi huo unashukuru sana kwa ushirikiano wa kamati hiyo katika kufanikisha zoezi hilo la fidia kwa wananchi.
Akizungumza katika mkutano huo, Mkuu wa Mkoa wa Mara Mheshimiwa Adam Kighoma Ali Malima ameeleza kuwa TAKUKURU waliagizwa kushughulikia tuhuma za ufisadi wa shilingi bilioni 5.1 kutoka malipo hewa na malipo yaliyoongezwa.
“Uchunguzi umeonyesha kulikuwa na vyote viwili, malipo hewa kabisa na mengine yaliyoongezwa thamani ili kuwanufaisha mafisadi wachache” alisema Mheshimiwa Malima.
Aidha ameeleza kuwa uchunguzi huo umebaini kuna baadhi ya nyumba ni mbovu sana wenyenyumba hizo wamelipwa pesa kubwa ikilinganishwa na nyumba nyingine ambazo ni nzuri lakini wamepewa malipo kidogo.
Mheshimiwa Malima amewapongeza maafisa kutoka TAKUKURU, Usalama wa Taifa, Jeshi la Polisi na vyombo vingine vya ulinzi na usalama kwa kufanikisha zoezi hilo muhimu sana kwa mustakabali wa taifa la Tanzania.
Wananchi 1639 wa vitongoji vinne vya vijiji vya Matongo na Bichune walianza kulipwa fidia iliyokadiriwa ya shilingi bilioni 33 kuanzia tarehe 20 Mei 2020 na tayari wengi wao wameshalipwa ambapo ndani yake TAKUKURU imebaini udanganyifu huo na uchunguzi bado unaendelea.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa