Ufaulu wa Mtihani wa Taifa wa Kumaliza Shule ya Msingi (PSLE) katika Mkoa wa Mara kwa mwaka 2023 umepanda ambapo jumla ya watahiniwa 52,731 sawa na asilimia 75 ya watahiniwa wote 70,182 waliofanya mtihani huo wamefaulu kwa kupata madaraja A, B na C.
Taarifa iliyotolewa na Kaimu Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Elimu Bwana Makwasa Bulenga imeeleza kuwa kati ya wanafunzi waliofaulu mtihani huo kwa mwaka 2023 wavulana ni 26,438 na wasichana ni 26,288.
Bwana Makwasa ameeleza kuwa mwaka 2022 Mkoa wa Mara ulikuwa na watahiniwa waliofaulu walikuwa 57,393 sawa na asilimia 74.53 ya wanafunzi wote waliofanya mtihani, ukilinganisha na mwaka huu ufaulu wa mwaka huu umepanda kwa asilimia 0.47.
“Wanafunzi wote walioanza darasa la kwanza mwaka 2017 walikuwa 90,300 ambapo kati yao wavulana walikuwa 44,900 na wasichana walikuwa 45,406 hata hivyo wanafunzi waliofanya mtihani huo walikuwa 70,182” amesema Bwana Bulenga.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa jumla ya watahiniwa 3,258 ambao ni sawa na asilimia 5.96 waliokuwa wameandikishwa kufanya mtihani katika Mkoa wa Mara hawakufanya kutokana na sababu mbalimbali.
Taarifa ya Bwana Bulenga imeitaja Halmashauri iliyofanya vizuri katika mtihani huo kuwa ni Manispaa ya Musoma, ikifuatiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Rorya, Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Halmashauri ya Wilaya ya Bunda na Halmashauri ya Mji wa Bunda.
Halmshauri nyingine ni Halmashauri ya Wilaya ya Musoma, Halmashauri ya Wilaya ya Butiama, Halmashauri ya Mji wa Bunda na ya mwisho ni Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti.
Mtihani wa Kumaliza Elimu ya Msingi umefanyika hapa nchini tarehe 13-14 Septemba, 2023 na matokeo yake kutolewa na Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA) tarehe 25 Novemba, 2023.
Wakati huo huo, Baraza la Mtihani la Tanzania limefungia vituo vya mtihani viwili (02) kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti Mkoa wa Mara vilivyothibitika kupanga kufanya udanganyifu katika mtihani huo mpaka hapo Baraza litakapojiridhisha kuwa ni salama kwa uendeshaji wa Mitihani ya Taifa.
Taarifa ya Baraza la Mitihani kuhusu matokeo ya mtihani wa Darasa la Saba,2023 imeeleza kuwa Baraza limechukua hatua hiyo kwa mujibu wa Sheria za Mitihani na kifungu 4 (8) cha Kanuni za Mitihani za Mwaka 2016.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa