Jumla ya wanafunzi 67,061 wa darasa la Kwanza sawa na asilimia 90.3 ya maoteo ya kupokea wanafunzi 74,224 wa kuanza darasa hilo wameandikishwa na kuanza masomo katika Mkoa wa Mara hadi kufikia tarehe 17 Januari, 2024.
Akizungumza na Waandishi wa Habari ofisini leo kwake, Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Said Mohamed Mtanda ameeleza kuwa kati ya walioandikishwa kuanza darasa la kwanza wavulana ni 33,319 na wavulana ni 33,742.
“Lakini pia kati ya wanafunzi wote walioandikishwa darasa la kwanza, wanafunzi 107 ni wenye mahitaji maalum na tayari wameanza masomo yao ”amesema Mhe. Mtanda.
Mhe. Mtanda ameeleza kuwa jumla ya wanafunzi 65,076 wameandikishwa darasa la awali ambapo wavulana ni 32,499 na wasichana ni 32,577 sawa na asilimia 78.7 ya maoteo ya kuandikisha wanafunzi 82,679. Kati ya wanafunzi wote walioandikishwa awali, wanafunzi 111 ni wenye mahitaji maalum.
Mkuu wa Mkoa ameeleza kuwa katika uandikishaji huo, jumla ya wanafunzi 503 wameandikishwa katika madarasa ya Mpango wa Elimu ya Msingi kwa Watoto Walioikosa (MEMKWA) ambapo wavulana ni 256 na wasichana ni 247.
Kwa upande wa kidato cha kwanza jumla ya wanafunzi 32,212 wameripoti shuleni sawa na asilimia 61.03 ya wanafunzi 52,782 waliofaulu na kuchaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2024 katika Mkoa wa Mara.
Mhe. Mtanda amewataka wazazi na walezi wenye watoto wanaotakiwa kuanza masomo kwa mwaka 2024 kuhakikisha wanawapeleka watoto wao shule kabla ya tarehe 31 Machi, 2024.
Aidha, Mhe. Mtanda amewataka viongozi wa ngazi mbalimbali kuhakikisha wanafanya msako na kuwachukulia hatua za kisheria wazazi na walezi wote wenye watoto wanaotakiwa kuanza shule ambao hawajaandikishwa.
Taarifa ya Mkuu wa Mkoa ni mwendelezo wa ufuatiliaji na tathmini ya ukaguzi wa shughuli za elimu katika Mkoa wa Mara kuanzia tarehe 8 Januari, 2024 baada ya kuanza muhula mpya wa masomo kwa mwaka 2024.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa