Mkuu wa Mkoa wa Mara Mheshimiwa Adam Kigoma Ali Malima amewataka watanzania kuendelee kumuombea Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ili aweze kuendeleza mazuri yote aliyokuwa akiyafanya marehemu Dkt. John Pombe Joseph Magufuli.
Mheshimiwa Malima amesema hayo wakati wa maombi maalum ya kumuombea Dkt. Magufuli na Mama Samia Suluhu Hassan yaliyoandaliwa na Kamati ya Maridhiano na Amani ya Mkoa wa Mara yaliyofanyika leo tarehe 7 Aprili 2021 katika Uwanja wa Mkendo, Manispaa ya Musoma.
“Tuendelee kumuombea Rais Samia ili awezekupata nguvu, ujasiri na uthubutu zaidi wa kuweza kuinyanyua Tanzania juu kimaendeleo” alisema Mheshimiwa Malima.
Ameeleza kuwa wakati tunaomboleza kifo cha Magufuli tuliona tumuombee pia Mheshimiwa Samia ili Tanzania iimarike zaidi kimaendeleo chini ya uongozi wake.
Mheshimiwa Malima ameeleza kuwa Marehemu Magufuli ameacha alama kubwa katika maendeleo ya Mkoa wa Mara na nchi ya Tanzania na mambo aliyoyafanya ni mengi ambayo yameacha historia kubwa kwa nchi yetu.
Wakati huo huo Mheshimiwa Malima amewataka wananchi wa Mkoa wa Mara kuachana na ukabila ambao unarudisha nyuma maendeleo ya mkoa huu na badala yake wananchi waungane katika kuiletea Mara Maendeleo.
“Mheshimiwa Magufuli alipokuja hapa mara ya mwisho katika uwanja huu huu (Mkendo) alituasa kuachana kabisa na ukabila kwani hauna tija yoyote katika maendeleo ya sisi wenyewe au ya mkoa wetu” alisema Mheshimiwa Malima.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Maridhiano na Amani ya Mkoa wa Mara Askofu Jacob Lutubija amewataka watu wote kumuombea Dkt. Magufuli ili Mungu aweze kumsamehe makosa yake na kumpumzisha katika amani yake.
“Wakati tunamuombea Dkt. Magufuli, ni wajibu wetu pia kumuombea Mheshimiwa Rais ili aweze kutekeleza majukumu yake kikamilifu kwa manufaa ya Mkoa wa Mara na Tanzania kwa ujumla” alisema Askofu Lutubija
Kamati ya Maridhiano na Amani inaundwa na viongozi mbalimbali wa madhehebu ya dini za kiislamu na kiktristu yaliyopo katika Mkoa wa Mara.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa