Wananchi wa Mkoa wa Mara wametakiwa kutumia maadhimisho ya Mara Day 2020 ili kujifunza mbinu bora za kilimo zitakazowasaidia kuwakomboa kiuchumi.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Mara Mheshimiwa Adam Kighoma Ali Malima wakati akizungumza na waandishi wa Habari ofisini kwake kuhusiana na maadhimisho ya Mara Day 2020 ambayo kwa upande wa Tanzania yatafanyika katika viwanja vya Mama Maria Nyerere vilivyopo katika Kitongoji cha Nyamigembe, Kijiji cha Butiama, wilayani Butiama kuanzia tarehe 12 hadi 15 Septemba 2020.
“Mwaka huu tumeunganisha Mara Day na maonesho ya kilimo, wananchi tutumie fursa hii kujifunza kuhusu kilimo bora na endelevu chenye tija ili tuweze kujikwamua kiuchumi” alisema Mheshimiwa Malima.
Aidha amewataka wakulima kutembelea na kupata mafunzo katika uwanja huo kwa mwaka mzima ili kuweza kupata mafunzo na ushauri kuhusu kilimo, ufugaji na uvuvi ili kuweza kuongeza tija katika shughuli zao.
Mheshimiwa Malima asemma shughuli zitakazofanyika katika Mara Day 2020 ni pamoja na upandaji miti na uwekaji wa becon katika eneo la Kirumi, kongamano la kimtandao litakalohusisha wadau kutoka Kenya na Tanzania, maonyesho na mafunzo ya kilimo yatakayofanyika katika viwanja vya maonyesho ya kilimo Butiama.
Mheshimiwa Malima pia amewataka wananchi wanaouzunguka Mto Mara kupunguza shughuli za kibinadamu katika eneo la mita sitini kuzunguka bonde la mto huo kwa mujibu wa sheria ya rasilimali za maji.
“Nimesikitishwa sana na ile clip inayoonyesha mwekezaji akiwafukuza wanyama wanaovuka Mto Mara kwenda Masai Mara nchini Kenya, lakini kama wadau tulikubaliana kuhusu kutoruhusu shughuli za kibinadamu kwenye kingo la Mto Mara ninategemea Serikali ya Kenya itachukua hatua za haraka kudhibiti hali hii” alisema Malima.
Uwanja wa maonyesho wa Mama Maria Nyerere una eneo la 120 umeandaliwa na Serikali ya Mkoa wa Mara kwa ajili ya kutoa mafunzo kwa wakulima ambalo limegawanyika katika maeneo ya ufugaji, uvuvi, kilimo na sehemu ya mafunzo.
Mara Day ni maadhimisho ya kuhamasisha shughuli za uhifadhi katika Bonde la Mto Mara ambalo linafanyika kwa kupokezana katika nchi za Kenya na Tanzania tangu mwaka 2012 na kilele ni tarehe 15 Septemba ya kila mwaka.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa