Tume ya Taifa ya Uchaguzi leo tarehe 20 Novemba, 2023 imekutana na wadau wa uchaguzi katika Mkoa wa Mara kwa ajili ya maandalizi ya uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura katika mkutano uliofanyika katika Wilaya ya Rorya.
Akizungumza katika kikao hicho, Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Bwana Ramadhani Kailima amewataka wadau wote kutoa ushirikiano katika kufanikisha zoezi hili la majaribio linalotarajiwa kufanyika kuanzia tarehe 24-30 Novemba, 2023.
“Lengo la na zoezi hili ni kuvifanyia majaribio vifaa na mfumo wa uchaguzi katika mazingira halisi ili kuweza kubaini changamoto kama zipo na kuzifanyia kazi kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2025” amesema Bwana Kailima.
Bwana Kailima ameeleza kuwa zoezi la uboreshaji litahusisha kuwaandikisha wananchi wa Tanzania wenye umri wa miaka 18 na zaidi na watakaotimiza miaka 18 kabla au ifikapo tarehe ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 na wapiga kura wanaoboresha taarifa zao.
Ameeleza kuwa Tume ya Uchaguzi inatarajia kutumia mfumo wa VRS katika uandikishaji wa wapiga kura na zoezi hilo litafanyika kuanzia saa mbili asubuhi hadi saa kumi na mbili jioni na kuwa Tume imejipanga kutumia njia mbalimbali kutoa elimu kwa wananchi.
Zoezi la majaribio la uboreshaji wa Daftari la Wagiga kura litafanyika katika Kata ya Ikoma, Halmashauri ya Wilaya ya Rorya Mkoa wa Mara na Kata ya Ng’ambo, Halmashauri ya Manispaa ya Tabora, Mkoa wa Tabora.
Bwana Kailima ameeleza kuwa jumla ya vituo vya kujiandikishia 16 vimetengwa kwa ajili ya zoezi hili ambapo vituo 10 vipo katika Kata ya Ng’ambo (Tabora) na vituo sita vipo katika Kata ya Ikoma (Mara) na vinaweza kuongezeka au kupungua kama kutakuwa na mahitaji ya kufanya hivyo.
Tume imekutana na wadau mbalimbali ikiwemo viongozi wa dini, viongozi wa vyama vya siasa, wahariri wa vyombo vya habari vya kijamii, viongozi wa vyama vya watu wenye ulemavu, waandishi wa habari, wazee maarufu na viongozi wa mila.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa