Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) Kanda ya Ziwa Mashariki leo imekabidhi dawa zenye thamani ya shilingi 23,000,000 kwa Mwakilishi Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara kwa ajili ya Magereza za Mkoa wa Mara.
Akikabidhi dawa hizo, Meneja wa TMDA Kanda ya Ziwa Mashariki Bi. Sophia Mziray ameeleza kuwa msaada huo wa dawa ni kwa ajili ya magereza zote za Mkoa wa Mara.
“Tunatambua kuwa kuna upungufu wa dawa katika magereza za Mkoa wa Mara, msaada huo utazisaidia magereza kuweza kutoa huduma kwa wafungwa na watu wengine wanaohudumiwa kiurahisi zaidi” alisema Bi. Mziray
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara ambaye pia ni Kaimu Katibu Tawala Msaidizi sehemu ya Afya Dkt. Juma Mfanga ameishukuru TMDA kwa msaada huo na kuitaka kuendelea kutoa msaada katika Mkoa wa Mara.
“Kuna upungufu wa dawa kwenye magereza zetu, kwa msaada huu tuliopokea leo zinaweza kuwasaidia walengwa wa dawa hizi” alisema Dkt. Mfanga.
Aidha Dkt. Mfanga ameitaka Jeshi la Magereza Mkoa wa Mara kutumia dawa hizo kulingana na matumizi yaliyokusudiwa.
Kwa upande wake, Kamanda wa Magereza Mkoa wa Mara Kamishna Msaidizi wa Magereza (ACP) Hospitus Mendi ameeleza kuwa TDMA Kanda ya Ziwa Mashariki ni wadau wao wakubwa na mara kwa mara wanakuja kutoa mafunzo mbalimbali katika magereza yaliyopo katika Mkoa wa Mara.
“Mara ya mwisho walitoa elimu katika magereza ya Mkoa wa Mara kuhusiana na namna ya kudhibiti ugonjwa wa Kifua Kikuu” alisema ACP Mendi.
Bwana Mendi ameeleza kuwa kwa dawa za kutumia katika magereza wanazipata zaidi kutoka kwa Kamishana wa Magereza nchini lakini kuna wakati hazitoshelezi mahitaji yao ya dawa.
Kamishna huyo Msaidizi ameeleza kuwa dawa hizo zilizotolewa msaada zitagawiwa katika magereza zote za Mkoa wa Mara ili ziweze kutumika kwa maksudi yaliyokusudiwa.
TMDA Kanda ya Mashariki inahudumia mikoa mitatu ambayo ni Mwanza, Simiyu na Mara na ofisi yake ipo katika eneo la Buzuruga, katika jiji la Mwanza.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa