TEHAMA KUONDOA MADALALI KWA WAKULIMA BUTIAMA
Wilaya ya Butiama imeanza kutumia jukwaa la Mobile Kilimo (M-Kilimo) kuwaondoa madalali wa mazao ya kilimo ili kuweza kuwanufaisha wakulima, wafugaji na wavuvi katika kuuza mazao yao.
Akitoa taarifa kwa Kiongozi wa Mbio Maalum za Mwenge wa Uhuru Kitaifa leo tarehe 26 Juni 2021, Kaimu Afisa TEHAMA wa Wilaya ya Butiama Bwana Julius Wambura amesema kuwa kwa kupitia jukwaa hilo mkulima, mvuvi na mfugaji anakuwa ameunganishwa na wanunuzi moja kwa moja.
“Jukwaa hili limeondoa wanunuzi wa kati (madalali) kwani mkulima anapata masoko na wanunuzi wa mazao yake moja kwa moja kupitia simu yake ya mkononi” alisema Bwana Wambura.
Ameeleza kuwa faida nyingine za jukwaa hilo ni kupata ushauri wa kitaalamu kwa wakati na kwa gharama nafuu na kuleta uwajibikaji wa kwa wataalamu wa kilimo kwa wateja ambao ni wakulima.
Aidha ameeleza kuwa jukwaa hili pia linapunguza usumbufu kutokana na uchache wa wataalamu na mkulima wa Butiama anaweza kuhudumiwa na mtaalamu yoyote anayetambulika kwenye ngazi ya kijiji, kata, wilaya au Wizara.
Bwana Wambura ameeleza kuwa jukwaa hilo linatumika katika shughuli mbalimbali kama vile kutangaza bidhaa, kutafuta masoko na kupata ushauri wa kitaalamu kwa kutumia simu ya mkononi.
Ameeleza kuwa jukwaa hili limeunganishwa katika kata zote 18 na vijiji 59 vya Wilaya ya Butiama na mpaka sasa unawakulima 31,606 waliosajiriwa kutumia mfumo huo.
Aidha Bwana Wambura ameeleza kuwa jukwaa hili linauwezo wa kuunganishwa katika aina yoyote ya simu ya mkononi ambayo mkulima atakuwa nayo.
Mwenge wa Uhuru ukiwa katika Wilaya ya Butiama umeweka jiwe la msingi katika Mradi wa Elimu Jumuishi Masafa katika kituo cha watu wenye ulemavu cha Lake Victoria Disability Centre; imeweka jiwe la msingi, kugawa vyandarua na kupanda miti katika Zahanati ya Mmazami; umezindua nyumba za mwekezaji.
Aidha Mwenge wa Uhuru umetembelea vizimba vya samaki vya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kikosi cha Rwamkoma; kupanda miti katika Chuo cha VETA na kutembelea mradi wa kisima cha maji kilichozinduliwa na Kiongozi wa Mwenge wa Uhuru mwaka 2019.
Hata hivyo mwenge wa uhuru umeikataa miradi miwili kutokana na dosari zilizojitokeza kwenye nyaraka na utekelezaji wa mradi hiyo.
Akizungumzia miradi hiyo Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Lt. Josephine Paul Mwambashi ameeleza kuwa katika mradi wa nyumba za polisi katika Kituo cha Polisi Kiabakari ameshindwa kuzindua kwa sababu hawakupata nyaraka yoyote kuhusiana na mradi huo.
Aidha katika mradi wa Ujenzi wa Chuo cha Mamlaka ya Elimu ya Ufundi Stadi (VETA) Bibi Mwambashi ameeleza kuwa Mwenge wa Uhuru umeshindwa kuweka jiwe la msingi katika mradi huo kutokana na sababu mbalimbali.
Amezitaja sababu hizo kuwa ni makadirio ya ujenzi (BOQ) yanayotumika hayaendani na ujenzi unaofanyika na inatofautiana idadi ya majengo, ukubwa wa baadhi ya majengo na gharama za mradi.
Ametoa mfano kuwa BOQ inayotumika kwenye mradi huo ambayo wameonyeshwa inagharama ya shilingi bilioni 1.6 wakati mradi unaotekelezwa kwa sasa unagharama ya zaidi ya bilioni 2.5.
“BOQ ya awali ilikuwa na majengo machache lakini idadi ya majengo na ukubwa wa majengo kwa sasa umeongezwa bila ya kutengeneza BOQ nyingine yenye uhalisia ya mradi huo” alisema Lt. Mwambashi.
Amezitaja kasoro nyingine kuwa ni kusosekana kwa uthibitisho wa mapokezi ya fedha; baadhi ya risiti za manunuzi ya vifaa kutokuwepo kwa ajili ya ukaguzi; kutokupima ubora wa vifaa vilivyotumika katika mradi huo; na ukubwa wa gharama katika baadhi ya majengo.
Amemuagiza Kamanda wa Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU) Wilaya ya Butiama kuchunguza mradi huo na kutoa taarifa za awali kabla Mwenge wa Uhuru haujaondoka Mkoa wa Mara tarehe 28 Juni 2021.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa