Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Kanali Evans Alfred Mtambi leo ameongoza maadhimisho ya sikukuu ya wafanyakazi katika Mkoa wa Mara yaliyofanyika katika uwanja wa mnadani, eneo la Kiabakari, Wilaya ya Butiama na kuwataka viongozi sehemu za kazi kutatua kero za watumishi kwa wakati ili waendelee kutekeleza majukumu yao badala ya kuzunguka na kufuatilia utatuzi wa changamoto zao.
“Wafanyakazi ni nguzo muhimu sana katika maendeleo ya nchi yetu, haipendezi kuwaona wakizunguka huku na huko kutafuta majibu ya changamoto zao kwa sababu wenye majibu hayo hawayatoi kwa wakati na kuwalazimisha watumishi kusafiri kufuatilia utatuzi wa changamoto zao” amesema Mhe. Mtambi.
Mhe. Mtambi amesema Serikali imechukua hatua nyingi sana ikiwemo kuboresha mishahara, kulipa madeni ya watumishi na kuwapandisha madaraja lakini wasimamizi sehemu za kazi wanapaswa kupunguza changamoto ndogondogo zilizopo katika maeneo yao ambazo zinawakatisha tama watumishi kufanyakazi.
Akizungumza katika maadhimisho hayo, Mhe. Mtambi amewataka watumishi kuongeza juhudi, weredi na maarifa hususan katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo ili miradi hiyo iweze kuleta manufaa yaliyokusudiwa katika jamii.
“Mhe. Rais anahangaika sana kutafuta fedha za kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo, tusipozitumia kwa namna zilivyokusudiwa na kwa wakati wananchi hawatapana huduma zilizotarajiwa kutokana na miradi hii” amesema Mhe. Mtambi.
Aidha, amewataka wafanyakazi kwa umoja wao kukemea ukatili wa kijinsia na mauaji katika jamii kwa kutoa elimu kwa wananchi kila wanapopata nafasi ya kufanya hivyo na kwa kufanya hivyo kunaweza kupunguza matukio ya ukatili na kujichukulia sheria mkononi katika jamii.
Amewataka viongozi wote kuanzisha operesheni maalum ya ukaguzi wa vyoo, usafi wa mazingira na matumizi ya maji safi na salama ili kukabiliana na ugonjwa wa kutapika na kuharisha uliopo katika Wilaya ya Musoma.
Mhe. Mtambi amewaagiza Wakurugenzi wa Halmashauri na wakuu wa taasisi za umma kuhakikisha kero za watumishi ambazo zipo ndani ya mamlaka zao kuzitatua na kuanza kuzishughulikia kuanzia leo ili kuboresha mazingira ya kazi ya watumishi.
Wakati huo huo, Mhe. Mtambi amewaahidi watumishi ambao hawakupata mshahara wa mwezi Machi, 2024 kutokana na kutokujaza taarifa katika mfumo wa taarifa za watumishi kuwa mshahara wao wa mwezi Mach, 2024 unashughulikiwa na Serikali na utalipwa hivi karibuni.
Mhe. Mtambi amesema kwa mwaka wa fedha 2022/2023 Serikali imelipa malimbikizo ya mishahara ya watumishi wa Sekretarieti ya Mkoa wa Mara na Halmashauri kiasi cha shilingi 995,417,127 na kuwaahidi watumishi Serikali itaendelea kulipa madai yao kila inapohitajika.
Mhe. Kanali Mtambi amewaagiza waajiri wote kuwasilisha michango ya pensheni za watumishi katika Mifuko ya Hifadhi za Jamii mapema iwezekanavyo ili kupunguza usumbufu kwa watumishi wakati wanastaafu au kuondolewa kazini kutokana na sababu mbalimbali.
Mkuu wa Mkoa ametoa muda wa mwezi mmoja taasisi zote za Mkoa wa Mara kuunda Mabaraza ya Wafanyakazi na kufanya vikao vya Mabaraza ya Wafanyakazi na kutoa taarifa za utekelezaji wa agizo hilo kwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara.
Mhe. Mtambi ameeleza kuwa Serikali imeajiri watumishi wapya 1,906 katika Mkoa wa Mara katika sekta za elimu, afya, kilimo na utawala na kuwataka watumishi hao wapya kutimiza majukumu yao na kufanyakazi kwa bidii.
Kwa upande wake, mwakilishi wa Mwenyekiti wa Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mara Mhe. Julius Masubo Kambarage amewapongeza wafanyakazi kwa kazi nzuri wanayoifanya na kuwahakikishia kuwa CCM inautambua mchango wao katika maendeleo ya nchi ya Tanzania.
Mhe. Kambarage amesema wabunge wa Mkoa wa Mara wameibeba ajenda ya kikokotoo na nyongeza za mishahara na maslahi ya watumishi na Chama cha Mapinduzi kinawapongeza sana kwa kazi wanayoifanya kuwatetea watumishi.
Mhe. Kambarage amesema CCM inajali watumishi wote kwa kuwa ni wadau muhimu sana katika maendeleo ya Taifa na kwa kuwa Serikali ya CCM ni sikivu, inayafanyia kazi maombi ya wafanyakazi kama yalivyowasilishwa katika vikao mbalimbali.
Mhe. Kambarage amewaomba watumishi kufuatilia hotuba itakayotolewa leo Mkoani Arusha ili kupata majibu stahiki ya maombi yao kutoka Serikali ya Chama cha Mapinduzi.
Kwa upande wake, Katibu wa TAMICO Bwana Ahmed Ngereza akisoma risala kwa niaba ya Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA) ameeleza kuwa wafanyakazi wa Mkoa wa Mara wanashukuru sana kwa nyongeza ya mshahara waliyoipata kwa mwaka 2023.
Bwana Ngereza amesema baadhi ya waajiri hawatoi kwa wakati makato ya pensheni kwa watumishi na hivyo kusababisha usumbufu kwa watumishi wanapostaafu au kuondolewa kazini kutokana na sababu mbalimbali.
Bwana Ngereza ameeleza kuwa baadhi ya waajiri hawawalipi watumishi wao fedha za kuwarudisha makwao kwa mujibu wa sheria jambo ambalo linasabasisha usumbufu kwa watumishi mara baada ya kuondoka ofisini.
Aidha, wafanyakazi wa Mkoa wa Mara wameiomba Serikali kutoa elimu ya namna ya kujaza taarifa zao katika mfumo wa PEPMIS na kusema kuwa mfumo umeongeza gharama kwa watumishi za kutafuta simu janja na mtandao na hususan watumishi wanaokaa maeneo ya pembezoni.
Kauli mbiu ya siku ya wafanyakazi duniani mwaka 2024 ni “Nyongeza ya Mishahara ni Msingi wa Mafao bora na kinga dhidi ya hali ngumu ya maisha” na kitaifa maadhimisho yamefanyika leo katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid Karume, Jijini Arusha na kuongozwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Isdori Mpango.
Maadhimisho ya siku ya Wafanyakazi Duniani Mkoa wa Mara yamehudhuriwa na Wakuu wa Wilaya, Katibu Tawala na Menejimenti ya Mkoa wa Mara, Mwakilishi wa Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Mara, Makatibu Tawala wa Wilaya, baadhi ya wabunge, Wakuu wa Taasisi za Umma, Wakurugenzi wa Halmashauri, watumishi wa umma na binafsi wa Mkoa wa Mara.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa