Mkuu wa Mkoa wa Mara Mheshimiwa Ally Salum Hapi ameitaka Halmashauri ya Wilaya ya Bunda kutatua changamoto mbalimbali zilizojitokeza katika utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Bunda.
Mheshimiwa Hapi ametoa agizo hilo leo tarehe 15 Agosti 2021 wakati alipofanya ziara katika Halmashauri ya Wilaya ya Bunda kukagua miradi ya maendeleo.
“Nakuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri kukutana na mafundi na vibarua waliokuwa wanajenga katika mradi huu siku ya Jumanne tarehe 17 Agosti 2021 ili kupata ufumbuzi wa madai yao ambayo wameyadai kwa muda mrefu sasa” aliagiza Mheshimiwa Hapi.
Aidha Mheshimiwa Hapi amemtaka Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo kufuatilia madai ya fidia ya mkazi wa eneo hilo ambaye familia yake ilihamishwa kupisha ujenzi wa hospitali hiyo.
“Huyu Mama inasemekana anadai shilingi milioni 22, Halmashauri ipate ushahidi wa uhalali wa deni hilo na kulilipa ili huyu mama apate haki yake kwa wakati apishe katika eneo hili” alisema Mheshimiwa Hapi.
Mheshimiwa Hapi pia ametoa mwezi mmoja wodi za wagonjwa ambazo fedha zake zilikuja tangu Machi 2021 ziwe zimekamilika kujengwa katika hospitali hiyo ili ziweze kuanza kutumika.
Aidha amepinga mapendekezo ya watendaji wa Halmashauri kuwa shilingi milioni 500 iliyopangwa kujenga wodi hizo hazitatosha kujenga wodi tatu na badala yake kuongeza zaidi ya shilingi milioni 200 na kuwataka watendaji hao kukamilisha ujenzi bila kuongeza fedha.
Mheshimiwa Hapi pia ameliagiza Shirika la Umeme nchini (TANESCO) kupeleka umeme kwenye majengo ya hospitali hiyo ifikapo tarehe 17 Agosti 2021 ili eneo hilo liweze kuwa na umeme.
Katika siku ya kwanza ya ziara yake katika Halmashauri ya Wilaya ya Bunda, Mheshimiwa Hapi ametembelea miradi miwili ya ujenzi wa barabara katika eneo la Iramba na Nyamswa, mradi wa ujenzi wa jengo la ofisi za halmashauri katika eneo la Kibara na mradi wa maji katika eneo la Iramba.
Aidha Mheshimiwa Hapi amezungumza na wananchi katika eneo la Iramba na Nyamswa na kuwataka watendaji kutatua changamoto za wananchi katika maeneo yao.
Katika ziara hiyo, Mkuu wa Mkoa ameambatana na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Mara Mheshimiwa Samweli Kiboye, Mkuu wa Wilaya ya Bunda Mheshimiwa Joshua Nassari na viongozi pamoja na watendaji wengine wa chama na serikali.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa