Mkuu wa Mkoa wa Mara Meja Jenerali Suleiman Mzee ameeleza kuwa hadi kufikia tarehe 15 Agosti, 2022 jumla ya bilioni 48.7 zimekwishatolewa na Serikali kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) kupitia Mpango wa Kususuru Kaya Maskini katika Mkoa wa Mara kuanzia mwaka 2014 hadi sasa.
Akitoa taarifa kwa wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Kufuatilia Ofisi za Viongozi wa Kitaifa ya Baraza la Wawakilishi na Maafisa kutoka Ofisi ya Makamu wa Pili ya Rais, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mheshimiwa Mzee ameeleza kuwa kwa sasa Mkoa una wanufaika kaya 63,346 kutoka katika Halmashauri zote za Mkoa wa Mara.
Mheshimiwa Mzee ameeleza kuwa kati ya fedha zilizotolewa, bilioni 42.856 ni kwa ajili ya malipo ya walengwa, shilingi bilioni 5.844 ni kwa ajili ya usimamizi na ufuatiliaji ngazi ya Mkoa, Halmashauri, Kata na ngazi ya Mitaa/Vijiji na shilingi milioni 283.542 ni kwa ajili ya miradi miwili ya maendeleo.
Katika taarifa hiyo, Mheshimiwa Mzee ameeleza kuwa uzinduzi wa utekelezaji wa sehemu ya pili ya TASAF awamu ya III ulifanyika tarehe 10 Agosti, 2021 katika Mkoa kwa lengo la kufikia asilimia 30 ya vijiji na mitaa ambayo haikuwa imefikiwa na sehemu ya kwanza ya TASAF III.
Mheshimiwa Mzee ameeleza kuwa kwa sasa jumla ya vijiji na mitaa 792 kutoka Halmashauri zote za Mkoa wa Mara zimeingia katika mpango huo huku vijiji 13 katika Wilaya ya Bunda (03) na Serengeti (10) havijafikiwa na Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Kusimamia Ofisi za Viongozi ya Baraza la Wawakilishi, Zanzibar Mheshimiwa Machano Othman Said amewataka wanufaika wa Mpang wa Kunusuru Kaya Maskini kutumia fedha wanazopata vizuri kwa maendeleo yao.
“Hii fedha mnayoipata mkiitumia vizuri itawasaidia sana katika kujiletea maendeleo yenu binafsi na maendeleo ya Taifa kwa ujumla” ameeleza Mheshimiwa Said.
Mheshimiwa Said ameeleza kuwa viongozi wa Serikali wanapambana kuhakikisha fedha hizo zinapatikana na kwamba wanufaika wakizitumia vizuri wataweza kufanya maendeleo yao na kuwatoa kabisa katika hali ya umaskini waliyokuwa nayo hapo awali.
Katika ziara hiyo, Viongozi hao walitembelea Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara, Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Butiama, wanufaika wa Kijiji cha Mlyaze katika Wilaya ya Butiama, Makumbusho ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Nyumbani kwa Baba wa Taifa katika eneo la Mwitongo, Butiama.
Katika ziara hiyo, viongozi hao waliambatana na maafisa wa TASAF kutoka Makao Makuu Dodoma, maafisa wa TASAF Mkoa wa Mara, maafisa kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara, Wilaya ya Butiama na Halmashauri ya Wilaya ya Butiama.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa