Serikali Mkoa wa Mara imedhibiti watu wasio Watanzania kujiandikisha au kuboresha taarifa zao kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwa kuwaelimisha wadau wa uchaguzi kusaidia katika udhibiti wa watu wasio raia na kuwasambaza maafisa uhamiaji katika vituo vya kujiandikishia.
Hayo yameelezwa na Mkuu wa Wilaya ya Tarime Meja Edward Gowele alipokutana na waandishi wa Habari ofisini kwake leo tarehe 7 Septemba, 2024 na kueleza kuwa Serikali inahakikisha wanaohusika tu ndio wanajiandikisha au kuboresha taarifa zao.
“Elimu imewasaidia wadau na hususan vyama vya siasa kujua kuwa ni jukumu lao kudhibiti watu kutoka nje ya Tanzania kujiandikisha maana watakuja kupiga kura na kuharibu uchaguzi wetu” amesema Meja Gowele.
Mhe. Gowele amesema zoezi la uandikishaji kwa Wilaya ya Tarime linaendelea vizuri mpaka sasa na mwitikio wa wananchi na hususan vijana wanaojiandikisha kwa mara ya kwanza ni mkubwa na katika baadhi ya vituo imelazimu kuongeza mashine na watumishi wanaohusika na uandikishaji.
Meja Gowele amesema Wilaya ya Tarime imeweka mikakati ya pamoja na Halmashauri zake mbili kuhusu namna ya kulikamilisha zoezi hili na kuwashirikisha wazee wa kimila, viongozi wa dini na viongozi wa vyama vya siasa.
Aidha, amesema Halmashauri zote mbili zimefanya matangazo ya kutosha kuhamasisha wananchi kushiriki na viongozi wa Serikali pia wamekuwa wakipita kwa wananchi kuwahamasisha ikiwemo na kwenye misiba.
Meja Gowele amewahamasisha wananchi wa Wilaya ya Tarime kutumia muda uliobakia kujitokeza na kuboresha taarifa zao katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura ambapo kwa Mkoa wa Mara mwisho wa zoezi hilo ni tarehe 10 Septemba, 2024.
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Sirari Mhe. Amosi Sagala Nyabikwi amesema amewahamasisha mawakala waliowekwa na Chama cha Mapinduzi (CCM) kudhibiti watu ambao sio watanzania kuboresha taarifa zao au kujiandikisha kuwa wapiga kura.
Mhe. Nyabikwi amesema Wenyeviti wa Vitongoji na wenyeviti wa Vijiji wamesaidia sana katika kuwabaini watu ambao sio wenyeji wa Tarime kwa kusikiliza wanavyoongea, kama hamna mtu anayemfahamu katika kitongoji husika na kwa kuangalia mambo mengine muhimu yanayowatofautisha Watanzania na watu wengine.
Kwa upande wake, Bwana Frank Marwa Yohana amesema vijana wengi wamehamasika na wanajitokeza kujiandikisha au kuboresha taarifa zao wakati huu kutokana na hamasa inayoendelea.
Bwana Yohana amesema vituo vingi vina foleni za watu wanaohitaji kujiandikisha na kuiomba Serikali kuongeza mashine na watumishi katika vituo ili wananchi wasitumie muda mrefu katika vituo vya kuboreshea taarifa zao.
Kwa upande wake, Wakala wa CCM katika kituo cha Sokoni, Sirari Bwana Mbassa Paulo Sasi amesema kuwa kituo hicho kipo jirani na mpaka ambapo raia kutoka nchi za jirani wamekuwa wanataka kuandikishwa kupiga kura Tanzania.
“Kwa sasa vigezo vingine vyote mtu akiwa navyo, tunaangalia chanjo ya ndui, Watanzania tunachanjwa kwenye bega lakini majirani zetu wanachanjwa kwenye mkono sio begani na kwa kutumia njia hii tunawakamata kiurahisi” amesema Bwana Sasi.
Bwana Mbassa amesema watu wanaokamatwa kwa njia hiyo wanakabidhiwa kwa Jeshi la Uhamiaji ambao wanapita vituoni mara kwa mara kwa ajili ya taratibu za kisheria.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa