Mkuu wa Mkoa wa Mara Mheshimiwa Ally Salum Hapi ameitaka Halmashauri ya Mji wa Tarime kurudisha fedha za wananchi au kuwapa maeneo ya kujenga vibanda vya biashara walivyoahidiwa ndani ya mwezi mmoja.
Agizo hilo limetolewa leo tarehe 13 Agosti 2021 na Mheshimiwa Hapi wakati akizungumza na viongozi na watumishi wa Wilaya ya Tarime katika ukumbi wa Chuo cha Ualimu Tarime.
Mheshimiwa Hapi amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Tarime kusimamia suala hilo na kuhakikisha wananchi wa Tarime wanapata haki yao ndani ya mwezi mmoja.
Awali akizungumza katika mkutano huo Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Mara Mheshimiwa Samweli Kiboye maarufu kama namba tatu ameeleza kuwa Halmashauri hiyo iliwachangisha watu fedha shilingi 450,000 mwaka 2017 kwa ahadi ya kupewa vibanda vya biashara.
“Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa tangu wakata huo mpaka leo wananchi hawajapata vibanda wala hamna majibu ya kueleweka kuhusu fedha zao walizotoa” alisema Mheshimiwa Kiboye.
Mheshimiwa Kiboye ameeleza kuwa matatizo kama hayo yanawachonganisha wananchi na Chama cha Mapinduzi kwa sababu ya uzembe wa watendaji wachache wanaichafua serikali.
Akizungumzia suala hilo Kaimu Mkurugenzi wa Mji wa Tarime Bwana Erasto Mbunga ameeleza kuwa wakati viwanja hivyo vya biashara vinatangazwa takriban wananchi 80 walilipia ambao bado wanadai mpaka sasa.
Bwana Mbunga ameeleza kuwa kwa sasa mradi huo ambao awali walipanga kuutekeleza ulisitishwa na serikali na kupangiwa majukumu mengine na hivyo bado walikuwa wanaangalia utaratibu wa kuwalipa wananchi.
Kikao hicho pia kilihudhuriwa na Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mheshimiwa Mwita Waitara ambaye pia ni Mbunge wa Tarime Vijijini kupitia Chama cha Mapinduzi.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa