Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (TANAPA) imeahidi kuiboresha Shule ya Msingi Kenyamusabi iliyopo katika Wilaya ya Tarime Mkoa wa Mara ikiwa ni sehemu ya maridhiano kati ya wananchi na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti (SENAPA).
Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Kanda ya Magharibi wa TANAPA Bwana Martin Loibooki ameeleza kuwa kwa kuanzia TANAPA itatoa shilingi milioni 10 kwa ajili ya kumalizia vyumba viwili vya madarasa vilivyoanza kujengwa kwa nguvu za wananchi katika shule hiyo.
“Mpango wetu ni kutenga fedha zaidi kwa ajili ya kujenga vyumba zaidi vya madarasa na kuyakarabati majengo ya shule yaliyopo katika bajeti ya TANAPA ya mwaka 2021/2022 ambayo inaendelea kuandaliwa” alisema Bwana Loibooki.
Aidha ameeleza kuwa TANAPA inampango wa kuendelea kuimarisha mahusiano na wananchi wa eneo hilo ambalo limekuwa na migogoro ya mara kwa mara kati ya wananchi na SENAPA kutokana na masuala ya kugombea mipaka, uwindaji haramu ndani ya hifadhi, wananchi kuharibu miradi iliyotengenezwa na SENAPA nakadhalika.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mara Mheshimiwa Adam Kighoma Ali Malima ambaye aliongoza kikao hicho cha maridhiano leo tarehe 3 Machi 2021 ameeleza kuwa wananchi wakishiriki ipasavyo kwenye ulinzi wa hifadhi ya Serengeti watafaidika na mambo mengi sana ikiwemo uboreshaji wa huduma za kijamii katika eneo hilo.
“Nimefurahishwa sana na TANAPA kukubali ombi la wananchi la kuiboresha shule hii ili wananchi na watoto wanaosoma hapa waone kuwa wanafaidika na kuwepo kwa hifadhi karibu na maeneo yao na sio hadithi tu”alisema Mheshimiwa Malima.
Aidha Mheshimiwa Malima amewahakikishia wananchi kuwa uchunguzi wa tukio la kupotea kwa Bwana Manga Kahuru Manga unaendelea na timu ya wataalamu wanaendelea kuchunguza na matokeo ya uchunguzi yatawasilishwa kwao mara baada ya uchunguzi kukamilika.
“Ninawaomba muendelee kutoa ushirikiano kwa timu ya uchunguzi wa tukio hilo ili tuweze kupata ufumbuzi wa tukio la kupotea kwa kijana huyu kwa haraka” alisema Mheshimiwa Malima.
Kijana Manga Kahuru Manga mwenye umri wa miaka 20 alipotea wakati akiwa anachunga ng’ombe na mwezie ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti tarehe 11 Desemba 2020 na mpaka sasa uchunguzi bado unaendelea.
Katika kikao hicho wananchi pamoja na diwani wa eneo hilo Mheshimiwa Ayoub Marwa walifurahishwa na ahadi hiyo ya TANAPA na kuahidi kutoa ushirikiano kwa TANAPA katika kuimarisha mahusiano yaliyopo kati ya hifadhi na wananchi wa eneo hilo.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa