Waziri Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mheshimiwa Suleiman Jafo amezitaka shule za sekondari za ufundi zilizopo hapa nchini kutoa elimu kwa vitendo, kufanyakazi kwa weledi na ubinifu ili kuweza kuwaandaa wanafunzi wanaosoma katika shule hizo kwa ajili ya Tanzania ya Viwanda.
Mheshimiwa Jafo ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na Maafisa Elimu wa Mikoa, Halmashauri na Wakuu wa Shule na walimu wapya walioajiriwa katika shule tisa za sekondari za ufundi zilizopo hapa nchini leo tarehe 22 Januari 2021 kupitia mtandao wa video.
“Shule hizi kwa sasa zimeboreshwa sana kuanzia miundombinu hadi wataalamu wa kufundisha hivyo ni matarajio yetu (TAMISEMI) kuwa zitajikita zaidi kwenye kufundisha kwa vitendo ili vijana wanaofundishwa watoke wakiwa wanaujuzi wa kutosha kuweza kutumika kwenye Tanzania yaViwanda” alisema Mheshimiwa Jafo.
Mheshimiwa Jafo ameeleza kuwa wakati serikali ya awamu ya tano inaingia madarakani kwa mara ya kwanza, shule hizi zilikuwa na miundombinu chakavu, hazina walimu wenye utaalamu wa ufundi na hazikuwa na vifaa vya kufundishia.
Mheshimiwa Waziri ameeleza kuwa kwa sasa shule hizi zimekarabatiwa na serikali imetumia shilingi zaidi ya shilingi bilioni 16 kukarabati shule hizi tayari serikali imeajiri wataalamu 150 wa ufundi mbalimbali kuanzia Novemba 2020 ambao tayari wapo mashuleni ili kuboresha ufundishaji katika shule hizi za ufundi.
Aidha Mheshimiwa Jafo ameahidi serikali kupeleka shilingi milioni 30 kwa kila shule ya ufundi kwa ajili ya kununua au kukarabati vifaa vya kujifunzia na kufundishia ili kuimarisha elimu inayotolewa katika shule hizo.
Aidha amezitaka halmashauri kuwalipa mara moja posho ya kijikimu walimu wote waliopangiwa katika hizi shule za ufundi ili waweze kujikimu wakati jitihada za kuingizwa katika mifumo ya mishahara zikiwa zinaendelea.
Mheshimiwa Waziri pia amewataka Wakuu wa Mikoa ambapo shule hizo zipo wawe walezi wa shule hizo na kusisimamia kwa ukaribu shule hizi ili ziweze kuleta manufaa yanayotarajiwa katika mikoa yao.
Mheshimiwa Jafo pia amewataka Wakuu wa Shule za Ufundi kuwahusisha mafundi mahiri waliopo katika mikoa yao katika ufundishaji wa wanafunzi kwa vitendo ili wanafunzi wanaosoma katika shule hizi waweze kufaidika na umahiri wa mafundi hao.
Shule za sekondari za ufundi hapa nchini ni pamoja na Shule ya Ufundi Chato (Geita), Shule ya Ufundi Mwadui (Shinyanga), Shule ya Ufundi Musoma (Mara), Shule ya Ufundi Moshi (Kilimanjaro) na shule ya Ufundi Bwiru (Mwanza). Shule nyingine ni Shule ya Ufundi ya Tanga (Tanga), Shule ya ufundi Iyunga (Mbeya), shule ya Ufundi Ifunda (Iringa) na Shule ya Ufundi Mtwara (Mtwara).
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa