Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) anayeshughulikia Elimu Dkt. Charles Msonde leo (Juni 20, 2024) ameanza ziara ya siku tano katika Mkoa wa Mara na kuwataka walimu kutekeleza majukumu yao kwa upendo, umahiri na uwajibikaji.
Akizungumza katika kikao kazi na wasimamizi wa elimu katika Wilaya ya Bunda Dkt. Msonde amewataka walimu kuongeza juhudi katika ufundishaji kwa darasa la tatu kwa shule za msingi na kidato cha kwanza kwa kuwa ndio madarasa ya ujuzi na umahiri ambayo kwa siku za hivi karibuni yamekuwa hayapewi kipaumbele katika ufundishaji.
“Tunajua walimu mmekuwa mnatumia nguvu kubwa sana kuwalazimisha watoto waelewe kwa haraka wakiwa darasa la nne na kidato cha pili wakati wakiwa katika madarasa ya nyuma walimu mliacha kuwaandaa” amesema Dkt. Msonde.
Amewataka walimu kutoa mwongozo mzuri kwa wanafunzi wa Kidato cha Kwanza kupenda kujifunza na kuzungumza lugha ya kiingereza, na kuwataka walimu kuacha kuzungumza Kiswahili katika masomo ambayo sio ya Kiswahili kwa shule za Sekondari.
Dkt. Msonde amesema Serikali imeendelea kushughulikia changamoto za walimu ikiwemo upandishaji wa madaraja na kulipa malimbikizo ya mishahara ya watumishi na kuzitaka Halmashauri kuwasilisha madai yote ya walimu Serikalini ili yaweze kulipwa kwa wakati.
Kwa upande wake, Kaimu Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Elimu Bwana Ayoub Mbilinyi Sektretarieti ya Mkoa wa Mara amemkaribisha na kummshukuru Dkt. Msonde kwa kufanya ziara katika Mkoa wa Mara na kuzungumza na wasimamizi wa Elimu katika Mkoa wa Mara.
Bwana Mbilinyi amemhakikishia Dkt. Msonde kuwa Sekretarieti ya Mkoa umeyachukua maelekezo yote ya Naibu Katibu Mkuu na inaenda kuyafanyia kazi ili kuleta mabadiliko chanya katika maendeleo ya elimu katika Mkoa wa Mara.
Kikao kazi hicho kilihudhuriwa na Maafisa Elimu kutoka ngazi ya Mkoa, Halmashauri ya Wilaya ya Bunda na Halmashauri ya Mji wa Bunda, Maafisa Elimu Kata na Wakuu wa Shule za Sekondari na Walimu Wakuu wa Shule za Msingi kutoka Halmashauri zote mbili za Wilaya ya Bunda.
Dkt. Msonde kesho anatarajiwa kuendelea na ziara yake katika Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti, Mkoa wa Mara.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa