Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara Bwana Gerald Musabila Kusaya leo katika ukumbi wa uwekezaji amefungua mafunzo ya Maafisa Tarafa na Watendaji wa Kata wa Mkoa wa Mara yaliyoandaliwa na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI).
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo yanayoendeshwa na wataalamu kutoka Chuo cha Serikali za Mitaa (HOMBOLO), Bwana Kusaya amewataka watumishi hao kusikiliza na kutatua kero za wananchi na kusimamia miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika maeneo yao.
“Ninyi ndio watendaji wakuu katika maeneo yenu ya kazi, ni kiungo muhimu kati ya Serikali na wananchi na majukumu yenu ni makubwa sana katika kuwahudumia wananchi na kuwaunganisha wananchi na Serikali yao” amesema Bwana Kusaya.
Amewataka watendaji hao kuisaidia Serikali katika kuibua miradi muhimu ya maendeleo katika maeneo yao, kutoa taarifa mapema ya uwepo wa changamoto, ajali au jambo lisilo la kawaida ili viongozi waweze kulifuatilia na kulifanyia kazi kwa haraka.
Bwana Kusaya amewataka watumishi hao kufanya kazi kwa kujiamini na kwa ufanisi kwa kuwa wanawawakilisha Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri katika maeneo yao na wakati wote maamuzi yao yasiwe ya kumuonea wala kumpendelea mtu bali kwa kufuata sera, sheria, kanuni na taratibu.
Katibu Tawala amewataka watumishi hao kusaidia katika kuwaelimisha wananchi kuhusu mafanikio ya serikali na miradi mbalimbali inayotekelezwa katika maeneo yao ikiwa ni pamoja na kuwahamasisha wananchi kushiriki shughuli za maendeleo na kuchangia katika miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika maeneo yao.
Bwana Kusaya ameeleza kuwa katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kuwatumikia wananchi kunakuwa na changamoto za utendaji na mahusiano baina ya viongozi ambazo zinazosababishwa na kutokujua majukumu na mipaka ya kila kiongozi katika utekelezaji wa majukumu yake.
Amewataka watumishi hao kushiriki kwa makini katika mafunzo hayo ikiwa ni pamoja na kutoa mifano na uzoefu wa kushughulikia changamoto za wananchi katika maeneo yao kwa kuwa mafunzo hayo ni shirikishi na yanafundishwa na wataalamu wabobevu.
Ameishukuru Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kwa kuandaa mafunzo hayo kwa watumishi na kuihakikishia kuwa yatakwenda kubadilisha utendaji wa watumishi hao katika kuwahudumia wananchi.
Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi wa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Bwana Ibrahim Pius Minja ameeleza kuwa mafunzo haya yanalenga kuwajengea uwezo watumishi hao ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.
“Mafunzo haya yatawawezesha kusikiliza, kutatua kero za wananchi, namna ya kuwasaidia kwa ufanisi viongozi wanaowawakilisha katika maeneo yao na kusimamia miradi ya maendeleo katika maeneo yao” amesema Bwana Minja.
Bwana Minja ameeleza kuwa mpaka sasa mafunzo kama haya yameshafanyika katika Mikoa 13 katika awamu ya kwanza nay a pili na katika hii awamu ya tatu mafunzo yatafanyika katika Mikoa ya Simiyu, Mara, Mwanza, Geita na Kagera na itabakia mikoa nane kukamilisha mikoa yote.
Bwana Minja ameeleza kuwa kwa awamu ya kwanza na ya pili walifanikiwa kutoa mafunzo kwa Maafisa Tarafa 240 na Watendaji wa Kata 1740 kutoka mikoa hiyo 13 ya awali.
Ameeleza kuwa ni matarajio ya Ofisi ya Rais TAMISEMI kuwa mafunzo haya yatawajengea uwezo na kuwawezesha kusimamia miradi ya maendeleo katika maeneo yao, kusikiliza na kushughulikia kero za wananchi na kuwaongoza na kuwahamasisha wananchi katika shughuli za maendeleo.
Bwana Minja ameeleza kuwa Maafisa Tarafa na Watendaji wa Kata wengi wameajiriwa hivi karibuni na hata walioajiriwa awali wanamuda mrefu hawajajengwewa uwezo wa kutekeleza majukumu yao kikamilifu na hivyo kushindwa kuwasaidia viongozi wao.
Kwa upande wake, Afisa Tarafa wa Tarafa ya Makongoro Wilaya ya Butiama Bibi Rebecca Joseph Mdodo ameishukuru Serikali kwa mafunzo hayo ambayo amesema yatawakumbusha kuhusu sera, sheria, kanuni na taratibu watakazozisimamia katika kuwahudumia wananchi katika maeneo yao.
Bibi Mdodo ameeleza kuwa mafunzo haya yatawaongezea ujuzi wa kuwa viongozi wazuri katika kuwatumikia, kuwasikiliza na kuwahudumia wananchi.
Aidha, Bibi Mdodo ameiomba Serikali kutoa mafunzo kazini kwa watumishi wa kada mbalimbali ili kuimarisha utumishi wao na hususan katika kusimamia miradi ya maendeleo na kuwaongoza wananchi katika kufikia maendeleo.
Ufunguzi wa mafunzo hayo umehudhuriwa pia na Maafisa kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI, Chuo cha Utumishi wa Umma, Chuo cha Serikali za Mitaa Hombolo, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara, Katibu Tawala wa Wilaya ya Musoma, Maafisa Tarafa na Watendaji wa Kata zote za Mkoa wa Mara.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa